October 6, 2024

Sababu za vijana kutochangamkia fursa za kujiunga na vyama wa wafanyakazi

Licha ya umuhimu wa vyama vya kutetea maslahi ya wafanyakazi, bado mwitikio wa wafanyakazi vijana kujiunga katika vyama hivyo ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa hamasa na elimu.

  • Baadhi yao wamesema hawana taarifa, hamasa na elimu ya kutosha kuhusu utendaji wa vyama hivyo. 
  • Wadau waeleza kuwa changamoto za uendeshaji ndani ya vyama hivyo ni kuzuizi kingine cha upatikanaji wa haki za wafanyakazi vijana.
  • Vijana washauriwa kujiunga na vyama hivyo ili kuwa sehemu ya kuboresha mazingira ya kazi. 

Dar es Salaam. Licha ya umuhimu wa vyama vya kutetea maslahi ya wafanyakazi, bado mwitikio wa wafanyakazi vijana kujiunga katika vyama hivyo ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa hamasa na elimu, Nukta imebaini. 

Mwongozo wa vyama vya wafanyakazi iliotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2016, unaeleza kuwa chama cha wafanyakazi ni umoja wa hiari na wa kidemokrasia unaoanzishwa na wafanyakazi wenyewe kutokana na mahitaji yao bila ya kushawishiwa na bila ya kuingiliwa na chombo chochote, kiwe cha Serikali au kinginecho.

Malengo makuu ya chama cha wafanyakazi ni kulinda na kupeleka mbele mahitaji na matakwa ya pamoja ya wafanyakazi yawe ya kiuchumi, kijamii, au kisiasa.

 “Mahitaji haya yanajumuisha uhakika wa ajira, malipo maridhawa ya ujira na marupurupu mengine, masharti bora ya kazi, na uboreshaji wa maisha ya mfanyakazi na wananchi kwa ujumla,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo.

Kwa Tanzania, vyama vya wafanyakazi vinasimamiwa na Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 ambapo kila mfanyakazi aliyeajirwa anayo haki ya kuunda na kujiunga na chama cha wafanyakazi pamoja na kushiriki katika shughuli halali za chama chake.

Miongoni mwa vyama vya wafanyakazi vilivyopo nchini ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) ambalo ni mwamvuli wa vyama vya wafanyakazi takriban 13 vya sekta mbalimbali ambapo linawachama takriban 650,000 hadi Juni 2016.

Vyama vilivyopo katika shirikisho hilo ni pamoja na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Chama cha Wafanyakazi wa Mahotelini, Mshambani na Majumbani (Chodawu) na Chama cha wafanyakazi wa Viwandani na Taasisi za Fedha (Tuico).

Wafanyakazi kwa hivyo wanastahiki malipo ya haki na usawa kwa nguvukazi wanayoitoa. Picha| ILO.

Hata wakati vyama hivyo na vingine vikitambulika kisheria, www.nukta.co.tz imebaini kuwa muitikio wa wafanyakazi vijana wengi kujiunga katika vyama hivyo ni mdogo na sababu kubwa ni uelewa mdogo walionao kuhusu vya vyama vya wafanyakazi katika kutetea maslahi yao mahali pa kazi.

Afisa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Mercy Masinga anasema amekuwa akisikia uwepo wa vyama vya wafanyakazi lakini hajajiunga kwa sababu hana ufahamu wa kutosha kuhusu umuhimu wa vyama hivyo. 

“Ni kweli sijajiunga kwa sababu sina uelewa wa shughuli zao na jinsi vinavyotumika kutetea maslahi ya wafanyakazi, labda nikielekezwa ninaweza kujiunga,” anasema Mercy.

Kutokujua haki za wafanyakazi mahali pa kazi, ni sababu nyingine inayowafanya vijana wasichangamkie vyama hivyo, licha ya kuwa vina mchango mkubwa katika kupigania haki zao ikiwemo mazingira bora ya kazi na ujira.

Wakati Mercy akisema hana taarifa za kutosha, wadau wengine wanasema vyama hivyo havijafanya uhamasishaji wa kutosha kuwashawishi wafanyakazi katika sekta mbalimbali kujiunga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vijana la Yopocode la jijini Dar es Salaam, Alfred Mwahalende anasema vijana wengi wako tayari kujiunga na vyama wafanyakazi lakini wamekosa msukumo wa kutosha wa kuanzisha na hata kujiunga na vyama vilivyopo.

Anabainisha kuwa wafanyakazi hasa wenye mikataba ya muda mfupi, wanapitia changamoto nyingi wakiwa kazini lakini hawafikiwi ipasavyo na taasisi zinazoweza kuungana na nao kupigania haki zao.

“Nilikosa msukumo na sikujua taratibu za vyama vya wafanyakazi,” amesema Mwahalende ambaye naye bado hajajiunga kwenye chama chochote kutokana na kukosa hamasa. 

Amebainisha kuwa baadhi ya vyama viko kwa maslahi fulani ambayo hayawanufaishi wanachama wao, jambo linalowafanya hata wale ambao hawajajiunga kusita kujiunga wakihofia kuwa maslahi yao hayatazingatiwa kwa mapana.


Zinazohusiana


Kutokana na mabadiliko ya hali ya kiuchumi, inadaiwa kuwa baadhi ya waajiri wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kudhoofisha vyama vya wafanyakazi ikiwemo kutoa rushwa ili kupunguza nguvu ya wafanyakazi kupigania mazingira na maslahi mazuri mahali pa kazi. 

“Niliwakaribisha site (kazini) kuja kuwahamasisha wafanyakazi lakini walikuja…tukajaza fomu lakini menejimenti ikawahonga wasifanye hivyo kukwepa ada za uanachama na harakati za maandamano,” amesema mdau mmoja wa ambaye anatokana katika kmapuni ya ujenzi ya jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mwongozo wa ILO unaeleza kuwa mwajiri hapaswi kuingilia na kukwamisha shughuli za vyama vya wafanyakazi na kama vinakiuka  sheria ziko taratibu za kufuata ili kutatua changamoto zinazojitokeza.

Mtaalam wa sheria kutoka kampuni ya Uwakili ya Extent Corporate Advisory (ECA), Nabiry Jumanne amesema bado wafanyakazi wana nafasi nzuri ya kutatua changamoto zao wakiwa kwenye vyama na ikishindikana wanaweza kwenda kwenye taasisi za usuluhishi.

“Mfanyakazi anapaswa kuwasilisha malalamiko yake juu ya ukosefu wa haki za msingi anazostahili kwa mamlaka ya chama hicho kwanza, na asiporidhika na majibu basi anaweza kwenda kwenye taasisi usuluhishi,” amesema Jumanne.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya ajira, wamesema siyo sahihi kuwa vijana hawajiungi katika vyama hivyo kwa sababu wao ndiyo nguvukazi kubwa katika shughuli nyingi za uzalishaji.

Aliyewahi kuwa Katibu wa mkoa wa Dar es Salaam wa Chama cha Wafanyakazi wa Mahotelini, Mashambani na Majumbani (Chodawu), Kassim Masimbo ameiambia www.nukta.co.tz kuwa dhana kwamba vijana wengi hawajiungi kwenye vyama vya wafanyakazi siyo sahihi.

Amesema wanaojiunga zaidi ni vijana na wanawake kuliko wazee lakini changamoto ya ukosefu wa fedha na mtawanyiko wa wafanyakazi, inakwamisha vijana kuingia katika vyama hivyo na hata wakiingia hawadumu muda mrefu.

Hata hivyo, wapo baadhi yao wanafahamu umuhimu wa vyama vya wafanyakazi lakini  hukimbilia kwenye vyama hivyo wakipata matatizo ikiwemo kufukuzwa kazi na kukosa haki zingine za marupuru na pensheni baada kukamilisha mikataba ya kazi. 

Wafanyakazi wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) wakiandamana katika maadhimisho ya Mei Mosi mwaka 2017 jijini Dar s Salaam. Picha|Gazeti la Rai.

Suluhisho ni kuongeza elimu na hamasa

Karibu wadau wote waliohojiwa na www.nukta.co.tz wanakubaliana kuwa vyama vya wafanyakazi ni muhimu lakini vinahitaji kujiimarisha zaidi kwa kuongeza hamasa na kutoa elimu zaidi katika maeneo ya kazi ili kuwasaidia wafanyakazi ambao hawajui haki zao.

Mwahalende anaeleza ili hilo lifanikiwa, vyama hivyo vinapaswa kupunguza changamoto hasa rushwa na kupigania zaidi maslahi ya wanachama wao waliopo katika maeneo mbalimbali ya kazi. 

Ili wafanyakazi wajenge imani na vyama vyao, vinashauriwa kuimarisha mfumo wa mawasiliano na kufanya kazi kwa uwazi na umoja ili kufikia matarajio yaliyowekwa.

Pia vinapaswa kushughulikia changamoto mpya ambazo zinasababisha vyama kubadilika kutoka kutekeleza shughuli za asili na kupanua maeneo mapya ya kufanyia kazi. Bila ya vyama kujibadili havitaweza kufanya kazi katika mazingira haya mapya ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia. 

“Muhimu zaidi katika kuyafikia matarajio ya wafanyakazi ni kiboresha mifumo ya mawasiliano,kwa njia mbalimbali za kisasa na za haraka, kutoa mrejesho kwa umma, kuboresha huduma kwa wateja na kwa kufanya hivyo wanachama au wafanyakazi watajenga imani na kujiunga na vyama,” anasema Masimbo.

Naye Mwanasheria Jumanne amesema ili kuongeza hamasa na nguvu ya vyama hivyo, vinatakiwa viunganishe nguvu na kuwa na ajenda inayoeleweka kwa wanachama wao na katika kuboresha maisha ya wafanyakazi Tanzania.

“Vyama vitengenezwe vikiwa na sera nzuri na za wazi za jinsi zitakavyoendeshwa na kusaidia wafanyakazi katika nyanja mbalimbali, pamoja na uwajibishwaji wa makosa yanayorudisha nyuma vyama hivyo,” anasema Jumanne.