October 7, 2024

Sababu za wanaume wengi kukasirishwa na kauli ya Chris Mauki

Kauli hiyo kaitoa katika kipindi kigumu cha corona na imeshindwa kujali wanaume wanaohatarisha maisha yao kwa ajili ya kuwatafutia wenzao wao.

  • Kauli hiyo kaitoa katika kipindi kigumu cha corona na huenda imewaumiza wanaume wengi wasiokuwa na vipato vya uhakika
  • Huenda andiko lake likaharibu zaidi ndoa au mahusiano ya watu badala ya kujenga.

Dk Chris Mauki, moja ya wanasaikolojia mashuhuri Tanzania, huenda ni miongoni mwa watu waliyoianza wiki vibaya.

Andiko lake kwenye mtandao wa Instagram halijapokelewa vyema na wanaume na kujikuta akishambuliwa vikali mtandaoni.

Katika andiko hilo Dk Mauki ameandika; “ukiona umeolewa na mume ambaye sentensi zake kutwa kucha ni “sina hela” au “kuna ishu fulani nafuatilia, ikitiki…” na jama anatoka asubuhi na kurudi jioni. Huna haja ya kuwahangaisha mitume na manabii wakuombee. Jua tu umeolewa na msanii #ChrisMauki.”

Kauli hiyo ya Dk Mauki imeumiza wengi nikiwemo mimi licha ya kwamba ameomba radhi na kuifafanua zaidi alichokuwa akimaanisha.

Ufafanuzi huo bado hauzuii kuitafakari kauli yake ya awali ambayo imefuatiwa na maandiko tofauti yanayoendelea kumjibu.

Wengi wameeleza hisia zao kuhusu andiko hilo lakini nami nitajaribu kueleza kwanini wanaume wengi wameguswa.

Kauli ya jumla jumla

Licha ya kuwa Dk Mauki ni mwanasaikolojia alijisahau na kuandika kitu kwa jumla jumla kiasi cha kumgusa na kumuumiza kila mwanaume awe ameoa au hajaoa. Nimeona vijana wenzangu lukuki ambao hawajaoa wakieleza kukwerwa na alichoandika.

Kwanini? Ujumbe alioundika unawapa kiburi wanawake na mabinti wasiokuwa na huruma na wenzi wao huku ukizidi kuwaongezea msongo wa mawazo wanaume wasio na vipato ambao kwa bahati mbaya husema maneno hayo kutokana na hali ngumu.

Wanaume huumia ndani kwa ndani

Lazima tutambue ukweli kuwa wanaume wengi si watu wa kueleza matatizo yao kwa watu na wakati mwingine ni vigumu kwa baadhi kuwajua wana matatizo kwa kuwa tangu tukiwa wadogo wamefundishwa kukabiliana na shida yeyote mbele yetu na kuacha “kulialia”.

Kauli kama “kuna mchongo nafuatilia” ni kawaida kwa wanaume wengi hata kama hana ili kutoikatisha tamaa familia yake hasa mwenza wake. Ni wachache sana ambao husema moja kwa moja “sina hela” ili kupunguza presha kutoka kwa mwenza wake.

Kuna wanaume huaga wanaenda kwenye mishe kumbe wanaondoka angalau kuzipa familia matumaini pamoja na ukweli kuwa hatarudi na kitu au ataishia kukopa kwa ndugu na marafiki. 

Dk Mauki hajawahi kusikia simulizi ya familia zenye njaa ambazo huchemsha nguo au mawe kuwapa matumaini watoto kuwa kuna chakula kinapikwa ili wapitiwe na usingizi, walale?


Zinazohusiana: 


Itaongeza msongo wa mawazo, sonona kwa wanaume

Hapana shaka kuna wanawake au mabinti ambao tayari wanauishi ujumbe wa Dk Mauki licha ya kwamba ameshaomba radhi na kufafanua.

Kauli hiyo itawapa viburi wanawake na kupeleka presha kwa waume zao au wapenzi wao za kutaka kuwahudumia kila wanachotaka licha ya ukweli kuwa hali ni ngumu.

Presha hizi zinaweza kuongeza msongo wa mawazo kwa wanaume wengi na kuonekana kuwa hawawezi kumudu mahitaji ya familia zao au wapenzi wao. Hakuna kitu kinachomuumiza mwanaume kama kuonekana ameshindwa kumhudumia mwenza wake licha ya mihangaiko yake yote.

Lazima tufahamu kuwa kuna wanaume wanavaa nguo moja wiki nzima ili kuhakikisha mke au mpenzi wake anapendeza. Kuna wanaume wanakula mlo mmoja au hawali kabisa ili kupata kidogo kwa ajili ya wenza wao.

Hawa wakikejeliwa na kauli kama za Dk Mauki wapo hatarini sana kupata matatizo ya afya ya akili. Wapo ambao huenda wakawaacha wake au wapenzi zao iwapo presha itazidi juu yao kuhusu fedha na hatimaye ndoa au mahusiano lukuki kuharibika.

Wanaume wengi hubaki na vitu moyoni vikiwemo vya hali ngumu ya kufanikisha kipato na mara nyingi hutoa kauli za matumiani kwa wenzi wao. Picha| Samuel Martins\Unsplash.

.

Amesema katika kipindi kigumu

Kauli ya Dk Mauki imetoka katika kipindi kigumu ambacho Taifa linakabiliwa na janga la ugonjwa wa corona (COVID-19). Kutokana na janga hilo lililoathiri sekta nyingi kiuchumi kuna wanaume wamepoteza kazi au biashara zao zimevurugwa kabisa kiasi cha kuyumbisha kabisa vipato vyao. 

Ni wazi wake za hawa wanaume wameshasikia kauli za “nasikilizia michongo” mara kibao.

Wanaume wengine wamemuona Dk Mauki kama mtu asiyejali hali za watu wenye kipato cha chini hasa katika kipindi hiki cha corona.

Maswali ambayo wengi wanajiuliza ni kwamba hivi kuna mtu mwenye fedha zake ataacha familia yake au mwenza wake ateseke? Hapana. Kuna watu wanaangaika kwa ajili ya wake zao. Wanafanya kazi hatarishi kwa ajili ya wapenzi wao.

Nakumbuka mwaka 2003 nikiwa katika vibarua vya kuvuna mpunga huko Mbarali kulikuwa na mzee wa makamu tuliyempa jina la “Lau nafasi” kutokana na kuimba wimbo huo wa Zilipendwa mara kwa mara. Mzee Lau alimtoroka mkewe na kusafiri kilomita 65 kuja kufanya vibarua vya kufyeka na kupiga mpunga ili apate fedha za kwenda kumhudumia mkewe na familia yake.

Mzee huyo wa miaka kama 60 hivi alikosa chandarua kambini lakini alilazimisha kulala kwenye mapigio ya mpunga akitafunwa na mbu huku muda wote akitueleza kuwa anataka akirudi “mke wangu afurahi.”

Ipo mifano mingi zaidi ya hata vijana ambao wapo tu kwenye mahusiano lakini wanawahudumia wapenzi wao kama wake zao. Kuna watu wanakula mikate ili kuwahudumia wapenzi wao ikiwemo kuwasomesha kwa kuungaunga na baadaye wanatoswa vilevile. Hawa watakuwa wamelia kabisa baada ya kusoma ujumbe wa Mauki.

Nafahamu kuna kesi chache za namna hiyo (outliers) za wanaume kukwepa majukumu ilihali wanapesa lakini haziwezi kutosha kuhalalisha kuwa wanaume wote wanaosema hawana fedha ni “wasanii”.

Kiufupi Dk Mauki anatakiwa awe anasoma zaidi ya mara tatu maandiko yake kabla ya hajayachapisha kwenye mitandao ya kijamii. Kutokana na umashuhuri wake nadhani kuna wakati atahitaji mhariri. Hii ni mara ya pili anaingia mgogoro na watumiaji wa mtandao kutokana na anachoandika.

Nafahamu hawezi kumfurahisha kila mtu lakini kuna maandiko mengi huumiza zaidi badala ya kuponyesha. Andiko la Dk Mauki limetonesha badala ya kutibu ndoa au mahusiano ya wanawake aliokuwa amewalenga.