November 24, 2024

Sababu zinazowazuia vijana kuchangamkia fursa za uzalisahaji kahawa Tanzania

Licha ya kuwa chanzo cha ajira cha maelfu ya watu, vijana hawaoni kilimo cha zao la kahawa kama fursa kwao kwani zao hilo linachukuwa muda mrefu kumnufaisha mkulima.

  • Ni pamoja na kuwa na kuwa na dhana potofu juu ya zao la kahawa.
  • Wengine wanakimbia kilimo hicho kutokana na kukosa mitaji.
  • Kahawa inahitaji uvumilivu ili kupata matokeo mzuri ya uwekezaji.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa zao la kahawa ni kati ya mazao maarufu ya biashara yanayolimwa nchini Tanzania, ushiriki wa vijana katika uzalishaji wa zao hilo umetajwa kuwa hauridhishi, jambo linalowazuia kufaidika na fursa lukuki zilizomo katika mnyororo wa thamani wa zao hilo. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Kilimo nchini (Annual Agriculture Sample Survey Initial Report 2016/17) ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zao hilo linalolimwa katika mikoa saba nchini ikiwemo Kilimanjaro, Songwe, Ruvuma na Mbeya na hutoa ajira takriban 183,343 kwa mwaka.

Licha ya kuwa chanzo cha ajira cha maelfu ya watu, vijana hawaoni kilimo cha zao la kahawa kama fursa kwao kwani zao hilo linachukuwa muda mrefu kumnufaisha mkulima.

Mratibu wa zao la kahawa katika Manispaa ya Moshi, Violet Kisanga amesema kwa sehemu kubwa zao hilo mkoani Kilimanjaro linalimwa na watu wazima huku vijana wakikataa kujihusisha nalo kutokana na dhana potofu walizonazo juu ya zao hilo.

“Vijana wanadhani kuwa kahawa bado mche unaanza kutoa matunda baada ya miaka mitatu kumbe hadi miche ya mwaka mmoja ipo,” amesema Kisanga.

Mdau huyo wa Kahawa kwa zaidi ya miaka 15 amesema vijana kushindwa kushiriki katika kilimo hicho inatishia uendelevu wa kilimo cha kahawa kwani wazee nao wanaenda wanachoka lakini wanakosa mrithi.

“Vijana wanatakiwa kuona kahawa kama fursa kwani kilimo chake kinaambatana na fursa endapo wakiwekeza. Wao wameenda shule hivyo wakiwekeza tofauti na sisi watafanya makubwa zaidi,” amesema Kisanga.

Wimbo usiosikika

Kwa vijana, huenda sauti za wadau wa kilimo cha kahawa zikahitaji vipaza sauti vingi zaidi kwani hamasa inayotolewa kwa sasa bado haijawafikia na kwa wengi, bado shingo zimeshupazwa.

Mkazi wa Moshi, Ben Bosco ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa shughuli ambazo vijana wanaziona zinawaingizia kipato ni biashara ya mitumba, kuajiriwa ama kujiajiri katika fani ya kusafirisha abiria kwa kutumia bodaboda.

Hata hivyo, kilimo wanachokifanya ni kile ambacho matokeo yake ni ya muda mfupi na kisichohitaji mtaji mkubwa kama ilivyo kwa kilimo cha kahawa.

“Kahawa na vijana haviendani, wengi wanaikwepa kwa sababu hailipi. Ukikuta kijana anajishughulisha na kilimo basi ni nyanya, vitunguu, karoti na mazao ya haraka,” amesema Bosco.

Hata vijana waliojitosa katika zao hilo ni wale ambao waamerithi kutoka kwa familia.

Kahawa inahitaji uvumilivu

Wakati unaiona kahawa katika kikombe, haimanishi ilitolewa shambani kisha kama mahindi ikasagwa na kuwa tayari. Wadau wa zao hilo wamesema inapitia hatua nyingi hadi kufikia kiwango cha kutumika mezani.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masoko ya kimikakati Manispaa Moshi John Benjamin, kahawa inahitaji mtu apige moyo konde kabla ya kunufaika nayo na kwa sasa vijana hawawezi kufanya hivyo.

Benjamin amesema vijana wanahitaji kipato cha haraka na ni vigumu kumshawishi kijana ambaye amesoma na kwenda chuo kikuu kurudi shambani kupambana na kahawa.

“Kahawa inahitaji hadi miaka mitatu kuanza kukupatia matunda. Hakuna kijana aliye na huo uvumilivu. Wengi wanaona bora wafanye biashara au wakaajiliwe,” amesema Benjamin.


Soma zaidi:


Mitaji ya uendeshaji wa mashamba ya kahawa ni kitendawili

Mtaalamu wa masuala ya masoko, Dorcas Mgogwe amesema kwa kijana ambaye hana hata mtaji wa kuanzia, kuanzisha shamba la kahawa ni vigumu kwani hata kama ana shamba la urithi, bado litahitaji kuandaliwa, kununua miche, kupanda na kadhalika na wengi ujuzi huo hawana.

“Kilio cha vijana katika masuala ya ajira ni  mtaji. Kijana atatoa wapi mtaji na kahawa kuendesha shamba lake sio haba. Utahitaji miche ya kupanda, uipande uihudumia ikiwemo mbolea na dawa. Kijana huyu tunayemuongelea ni “fresh graduate” (mhitimu wa hivi karibuni) na hana kipato. Lazima akaajiliwe,” amesema Mgogwe.


Dhana potofu miongoni mwa vijana

Vijana nao wameendelea kuambizana habari ambazo huenda hazina ukweli miongoni mwao dhidi ya zao la kahawa na ni chanzo cha baadhi yao kutokuwaza kujihusisha na kilimo hicho.

Mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya mawasiliano kutoka Dar es Salaam ambaye ni mzaliwa wa Kilimanjaro Mike Roosevelt amesema kumekuwepo minong’ono kuwa kilimo cha kahawa kimesababisha wazee wengi waliojihusisha nacho kufariki kwa saratani.

“Wazee wengi kwa Moshi wamefariki na ugonjwa wa saratani hivyo vijana huunganisha vifo vyao na shughuli ambazo walikuwa wakifanya na wengi walikuwa wakijihusisha na kilimo cha kahawa,” amesema Roosevelt.

Hali hiyo inawafanya vijana wengi kutafuta shughuli zingine za kufanya na kukwepa kilimo cha kahawa kwa kuhofia kupata vifo kama vya wazee wao.

Hata hivyo, vijana wameshauriwa kubadili mtazamo huo potofu na kuangalia namna ya kuwekeza katika zao la kahawa ikizingatiwa mahitaji ya soko la ndani na nje yapo, jambo linaloweza kuwapatia kipato cha kukidhi maisha kuliko kusibiri kuajiliwa.