July 8, 2024

SADC yazungumzia Tanzania kuingia uchumi wa kati

Yazitaka nchi zingine za jumuiya hiyo kuongeza kasi ya maendeleo ili zifikie uchumi wa kati kama Tanzania.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azzan Zungu akifungua Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa njia ya mtandao, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Isidor Mpango, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.


  • Yaipongeza Tanzania kuingia uchumi wa kati.
  • Yazitaka nchi zingine za jumuiya hiyo kuongeza kasi ya maendeleo. 

Dar es Salaam. Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezipongeza nchi za Tanzania na Mauritania kwa kufanikiwa kuingia katika uchumi wa kati na juu licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi zilizoikumba jumuiya hiyo.

Benki ya Dunia iliiorodhesha Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati mwanzoni mwa mwaka huu sambamba na Mauritania kupandishwa daraja na kuwa nchi yenye kipato cha juu kutokana na kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja.

“Kwa Tanzania pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka dola za Marekani 1,020 (Sh2.4 milioni) kwa mwaka 2018 na kufikia dola za Marekani 1,080(Sh2.5 milioni) kwa mwaka 2019.

“Mauritania pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka hadi kufikia dola za Marekani 12,740 (Sh29.5 milioni) kwa mwaka 2019 kutoka na dola za Marekani 12,050 (Sh27.9 milioni) mwaka 2018”, amesema leo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu alipofungua Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa nchi za SADC.

Zungu alikuwa akimuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Isdor Mpango katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC), Jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi: 


Zungu amesema pamoja na Tanzania kupanda daraja hakuna nchi mwanachama ambayo imeshuka daraja na kuzishauri nchi wanachama kuyatumia mafanikio hayo kama chachu ya kujitathmini na kuangalia uwezekano wa kuleta maendeleo zaidi ya kiuchumi katika nchi za SADC.

Pia alizisihi nchi wanachama kuendelea kuchukua hatua za kukabiliana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) bila kuathiri shughuli za kiuchumi kwa kuwa ugonjwa huo ni changamoto nyingine ya uchumi wa jumuiya hiyo.

“Matokeo ya uchambuzi wa athari za ugonjwa wa COVID-19 kwenye viashiria vya muunganiko wa uchumi mpana kwa nchi za SADC yameonesha nchi wanachama zinatarajia kushuhudia ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti ya Serikali na kuongezeka kwa madeni”,amesema Zungu.

Zungu amezishauri nchi wanachama wa SADC kutafuta fedha kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu ili kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijami ambazo ziliatharika na COVID-19 pamoja na kupunguza mzigo wa madeni.