November 24, 2024

Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 uongozi Tanzania

Idadi ya wanawake wanaochaguliwa katika nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge bado iko chini. Mila potofu, mfumo dume na umaskini wa kipato wachangia kuwadidimiza.

  • Idadi ya wanawake wanaochaguliwa katika nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge bado iko chini.
  • Mila potofu, mfumo dume na umaskini wa kipato wachangia kuwadidimiza.
  • Mabadiliko ya sheria na kujiamini vitawasaidia kuwapatia nafasi nyingi za uongozi. 

Dar es Salaam. Huenda hamasa waliyonayo wanawake kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka huu ili kupata nafasi za uongozi na kuingia katika vyombo vya maamuzi isitimie kutokana sababu mbalimbali ikiwemo umaskini wa kipato unaowakabili.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 28 utawapa Watanzania fursa ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani. 

Wanawake wamekuwa ni kundi muhimu kwenye jamii, licha ya kuwa wanakabiliwa na changamoto lukuki kutumia uwezo na ujuzi wao kufanikisha ajenda za maendeleo. 

Kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya watu Tanzania kwa mwaka 2020 yaliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya wanawake ni milioni 29.4 sawa na asilimia 51.1 ya Watanzania wote milioni 57.6 waliopo sasa.

Wingi wa wanawake waliopo nchini bado haujawezesha usawa wa jinsia katika nafasi za uongozi zinazotokana na uchaguzi ili kufikia dhamira ya asilimia 50 kwa 50 kwa wanawake na wanaume. 

Hilo limekuwa likijidhihirisha katika chaguzi zinazofanyika nchini kila baada ya miaka mitano, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kwa  Tanzania kutokomeza umaskini na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi inayopawa wananchi haki ya kuchagua kiongozi wamtakaye.

Takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), zinaonyesha kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015,  idadi ya wanawake waliopata nafasi za uongozi katika Bunge la Tanzania kupitia majimbo, viti maalum na uteuzi wa Rais ilikuwa ni 126 sawa na asilimia 32 ya wabunge 393 wote walioingia Bungeni mwaka huo.

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila Wabunge 10 wa Bunge hilo waliokuwepo katika kipindi hicho, basi takriban watatu walikuwa ni wanawake.

Kwa Zanzibar wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi 2015 kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni asilimia 36 au wawakilishi 28 kati ya 84 huku wanawake waliopata nafasi za udiwani ni 85 kati ya 173 ikiwa ni nafuu kidogo ikilinganishwa na nafasi za uwakilishi.

Hata hivyo, idadi ya wanawake wanaoshiriki katika vyombo vya maamuzi imekuwa ikiongezeka lakini siyo kwa kasi ya kuridhisha.

Takwimu za NEC zinaonyesha kuwa  mwaka 1995, wakati wa uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi, ni wanawake nane tu waliojitosa majimboni ambao walishinda ubunge, wanawake 37 walipata ubunge kupitia nafasi za viti maalumu.

Idadi hiyo ikawawezesha wanawake 45 (asilimia 16) kuingia Bungeni kati ya Wabunge 269 waliochaguliwa wakati huo. Idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia asilimia 36 mwaka 2010 kabla haijashuka hadi asilimia 32 katika uchaguzi wa 2015.

Takwimu hizo zinabainisha wazi kuwa kuna kibarua kigumu kwa wanawake kupata fursa sawa kijinsia katika utawala na utoaji maamuzi katika Bunge, Baraza la Wawakilishi na kwenye Halmashauri za Wilaya. 

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben akifungua mafunzo ya asasi tatu za Kiraia zinazotekeleza mradi wa Wanawake Sasa za TAMWA, GEPF na Wildaf lAgosti 10, 2020 kuhusu Tathmini na Ufuatiliaji ili kuongeza  ufanisi katika ufanyaji tathmini wa masuala ya Jinsia. Picha|TAMWA.


Nini kinawakwamisha wanawake?

Hivi karibuni Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) na shirika la Global Peace Foundation (GPF) kiliendesha midahalo ya wanawake na wadau wa siasa iliyolenga kuibua mjadala wa ushiriki wa wanawake uchaguzi ili kupata nafasi za uongozi.

Chini ya mradi wa “Wanawake Sasa”, midahalo hiyo iliyowakutanisha wanawake 120 na kutoka vyama vya siasa vitano na kuibua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wanawake kupata nafasi za kuchaguliwa na kuteuliwa katika uchaguzi wa mwaka huu ambao utatoa dira ya maamuzi ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

Wanawake wanakabiliwa na changamoto za kipato na rasilimali fedha kuendesha shughuli za uongozi na uchaguzi na kuwafanya wakate tamaa ya kushiriki kikakimalifu katika kuzifikia ndoto zao.  

“Mwanamke haruhusiwi kurithi mali, mawazo yake yanakuwa hayathaminiwi, pia mila na desturi zinadhoofisha nafasi ya mwanamke kushiriki fursa za uongozi kwa sababu ya mtazamo hasi  juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii,” anasema Msimamizi wa mradi wa “Wanawake Sasa”, Sylivia Daulinge. 

Baadhi ya wanawake walioshiriki katika midahalo hiyo akiwemo Asya Mwadini Mohamed kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema-Zanzibar) wamesema wanatishiwa kupewa talaka, kupigwa na mwenzi wao na kuonekana wahuni na malaya pale wanapotaka kutumia haki yao ya msingi ya kuchaguliwa. 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi haki za wanawake za kushiriki katika uongozi hasa katika  Ibara ya 21 inayosisitiza kuwa kila raia wa Jamhuri ya Muungano ana haki sawa ya kushiriki katika uongozi wa nchi aidha moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi.

Pia kubaguana na kutokokuwezeshana miongoni mwa akina mama ni sababu nyingine inayowarudisha nyuma katika kushika hatamu za uongozi, jambo linalowafanya waendelee kulalamika na kusubiri kuteuliwa nafasi za viti maalum. 

“Mwanamke kiongozi  haonekani kama ni msaada wa kuwanyanyua wanawake wengiine,” anasema Daulinge na kubainisha kuwa suala hilo ni matokeo ya wivu na majivuno kwa viongozi wanawake dhidi na wanawake wenzie.

Vyombo vya habari kutoa upendeleo kwa wanaume zaidi kuliko wanawake kwa kigezo cha fedha(rushwa na mtazamo hasi wa vyombo vya habari kwa wanawake, kuandikwa vibaya kwenye magazeti, kudhalilishwa kupitia mitandao) nako kumelalamikiwa na wanawake kuelekea Uchaguzi Mkuu. 

“Changamoto za kiisakolojia nazo zinachangia ikiwemo kukosa uwezo wa ndani, kutokujiamini, kuhofia mila na desturi. Pia kukosa mafunzo na makuzi ya uongozi kuanzia ngazi ya chini ya malezi,” anasema.


Zinazohusiana: 


Matumaini yapo mwaka huu?

Licha ya hamasa inayotolewa kuwahimiza wanawake kugombea nafasi ya uongozi, huenda wanawake wakaendelea kuachwa nyuma katika nafasi za uongozi kutokana na idadi ndogo ya wanawake waliochaguliwa kupeperusha bendera za vyama vyao katika nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi katika uchaguzi wa mwaka huu. 

Mathalani, Katika majimbo 264 ya Ubunge ambayo yatashiriki uchaguzi, CCM imewateua wanawake 27 ambapo sita wanatoka Zanzibar watapeperusha bendera ya chama hicho katika majimbo ya uchaguzi.

Hiyo ni sawa na kusema asilimia 10.2 ya wagombea wote wa Ubunge wa chama hicho ni wanawake, huku wanawake wengine watatakiwa kusubiri kuteuliwa katika nafasi ya viti maalum kutegemeana na ushindi wa chama hicho baada ya uchaguzi. 

Katika orodha iliyotolewa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni chama kikuu cha upinzani, inaonyesha wanawake 50 wameteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya Ubunge na uwakilishi katika uchaguzi wa mwaka huu.

Azimio la Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) la maendeleo na usawa la mwaka 2008, linataka ushiriki wa wanawake na wanaume katika fursa za uongozi kuwa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030 kwa nchi wote wanachama ikiwemo Tanzania.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan (Wa tatu kutoka kushoto) akizungumza na ujumbe wa Mtandao wa Wanawake, Katiba na Uongozi  uliomtembelea Makamu wa Rais na kuzungumza nae Ikulu jijini Dar es Salaam na kujadiliana nae masuala mbali mbali yanayohusu changamoto za mtoto wa kike na mwanamke hivi karibuni. Picha\WFT-TRUST. 

Mikakati ya kuwasaidia wanawake

Washiriki wa midahalo hiyo wamependekeza kuunda au kuboresha mfumo wa kisheria na sera ili kutoa nafasi mahususi kwa ushiriki wa wanawake katika uongozi na kufanya maamuzi ikiwemo kutunga sheria ambayo inahitaji vyama vya siasa kutekeleza upendeleo wa kijinsia katika uteuzi wa wagombea.

Wanawake wametakiwa kujiamini na kutobaki nyuma hasa yanapojitokeza masuala yanayogusa maslahi yao ili kuwa sehemu ya maendeleo ya jamii. 

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben amesema wanawake walioteuliwa kugombea nafasi kupitia vyama vya siasa wasaidie kuhakikisha wanapata nafasi za uongozi ili waingie katika vyombo vya maamuzi.

“Vyama vya siasa vilivyotoa nafasi kwa wanawake viendelee kuwasimamia ipasavyo ili wafikie lengo, inawezekana!,” amesema Reuben hivi wakati akifungua mafunzo kuhusu kuongeza  ufanisi katika ufanyaji tathmini wa masuala ya jinsia jijini Dar es Salaam. 

Naye mwanaharakati wa masuala ya kijinsia, Anna Marie amesema “tuwajengee uwezo wanasiasa Wanawake wazungumze wawapo bungeni. Tusiishie kuwapa elimu na kuhamasisha washiriki katika siasa tu; bali tuwasaidie kuzungumza na kuibua hoja za msingi wawapo katika ngazi za maamuzi.”