October 6, 2024

Safari bado ndefu magari ya gesi asilia Tanzania

Licha ya kuwa magari yanayotumia gesi asilia yanaokoa uharibifu wa mazingira na gharama za maisga kwa kupunguza gharama za mafuta mafuta, bado muitikio wa Watanzania kutumia magari hayo ni mdogo.

  • Mpaka sasa magari yasiyozidi 400 ndiyo yanatumia mfumo wa gesi asilia nchini.
  • Changamoto kubwa ni mtazamo hasi na upungufu wa vituo vya kujazia gesi asilia.
  • Serikali yasema imejiwekea mikakati mbalimbali kuchagiza matumizi ya gesi asilia kwenye magari.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa magari yanayotumia gesi asilia yanaokoa uharibifu wa mazingira na gharama za maisha kwa kupunguza gharama za mafuta, bado muitikio wa Watanzania kutumia magari hayo ni mdogo kutokana na ukosefu elimu kuhusu umuhimu wa magari hayo.

Mratibu wa mradi wa ufungaji wa mifumo ya gesi asilia (CNG) kutoka Taasisi ya Teknolijia ya Dar es Salaam (DIT), Dk Esebi Nyari amesema tangu mradi huo uanze mwaka 2008 wamefanikiwa kufunga mfumo wa gesi asilia kwenye magari yasiyozidi 400 nchi nzima.

Gesi asilia ni nishati safi na salama kwa magari ambapo bei yake iko chini ukilinganisha na petroli na humuwezesha dereva kutembea umbali mrefu kwa kutumia kiwango kidogo cha gesi.

Baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo hasi kuhusu matumizi ya gesi hiyo kwenye magari kwa kila kile wanachoamini kuwa gesi hiyo inaweza kulipuka na kuleta madhara ikiwemo gari kuungua au kuharibika.

“Gesi hii ni salama. Watu wengi wanakuwa na hofu kuwa wakifunga gesi hii gari litalipuka. Tabia ya gesi hii ni tofauti na gesi ya kupikia nyumbani… haishiki moto haraka, ni nyepesi na hairuhusu kutengeneza moto ikivuja tu inayeyuka haraka hewani,” anasema Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Mitambo wa DIT, Gerutu Bosinge.  

Pia DIT na wadau wengine bado wana kibarua kigumu cha kuishawishi Serikali kuongeza vituo vya kujazia gesi asilia ikizingatiwa kuwa kuna kituo kimoja mpaka sasa ambacho kinapatikana Ubungo, Jijini Dar es Salaam.

Hali hiyo imekuwa ikipunguza kasi ya watu kufungiwa mfumo wa gesi asilia kwenye magari yao hata wale waliofungiwa mara gesi inapoisha hugeukia matumizi ya petroli ambayo hupandisha gharama zao za maisha na biashara. 

Bosinge anasema kama vituo hivyo vitajengwa katika maeneo mbalimbali nchini vitafungua fursa za ajira kwa vijana na kuongeza idadi ya magari yanatumia gesi asilia.


Zinazohusiana:


Serikali yatoa mwanga wa matumaini

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza gesi asilia kwa lengo la kuhakikisha gesi hiyo inatumika kwa matumizi mbalimbali yakiwemo ya viwandani, majumbani, kwenye magari na kuzalisha umeme.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linakusudia kujenga kituo mama cha kupunguza mgandamizo wa gesi asilia (Compressed Natural Gas – CNG Mother Station) chenye kituo cha kujazia gesi kwenye  magari eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aidha, vituo vidogo vya kupunguza mgandamizo wa gesi asilia (CNG Daughter Stations) vitajengwa maeneo ya Hospitali ya Muhimbili (MNH), Soko la Samaki Feri na Ubungo. Kituo cha Ubungo kitatumika kujaza gesi katika Mabasi ya Mwendokasi zaidi ya 300 pamoja na magari mengine zikiwemo daladala ikiwemo ni sehemu ya magari yatakayobadilishwa hapo baadaye. 

“Katika kuendelea na juhudi za kuwezesha mikoa mingine nchini kunufaika na rasilimali ya gesi asilia, Serikali itaendelea kufanya tafiti za namna bora ya kuunganisha mikoa hiyo na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza rasilimali hiyo,” alisema Waziri wa Nishati, Dk Merdad Kalemani wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake ya 2019/2020.

Baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo hasi kuhusu matumizi ya gesi hiyo kwenye magari kwa kila kile wanachoamini kuwa gesi hiyo inaweza kulipuka na kuleta madhara ikiwemo gari kuungua au kuharibika. Picha|Emirates Business.

Kwa kuanzia, usambazaji wa gesi asilia unatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Pwani, Tanga, Morogoro, Dodoma, Kilimanjaro, Mwanza na Arusha ambapo kwa mujibu wa Dk Kalemani, mpango huo unatarajiwa kutekelezwa kati ya sasa na mwaka 2025.

“Kwa hiyo kwa Mtanzania wa kawaida anaweza kutumia; kama tumeweza kutumia e-passport (Pasipoti za kielektroniki) wanazotumia wasafiri basi ni wakati wa kuanza kutumia gesi asilia kwenye magari,” anasema Mhandisi Bosinge na kuongeza kuwa,

“Dunia ya sasa inatafuta namna ya kutumia nishati endelevu inayosaidia kurahisisha maisha na hatuwezi kukwepa huko tuendako, ni vema tukaanza mapema.”

Kwa mujibu wa Kituo cha Mipango na Masomo ya Kimataifa (CSIC) ni asilimia 2 ya magari yote duniani ndiyo yanatumia gesi asilia ambapo kuna vituo 32,211 vinavyojaza gesi hiyo kwenye magari na kati ya hivyo 210 vinapatikana Afrika. 

Nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutumia teknolojia ya magari ya gesi asilia ni pamoja na China, Marekani, Brazil na Argentina ambapo kwa Afrika matumizi makubwa yapo Afrika Kusini, Msumbiji na Misri.