November 24, 2024

Safari bado ndefu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu

Utekelezaji wake unakwamishwa na kutokuwepo kwa usawa, athari za utandawazi na mabadiliko ya teknolojia.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres akizungumza jana (Julai 15, 2019) jijini New York, Marekani ambako Tanzania itawasilisha ripoti yake katika ufunguzi wa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la mawaziri (HLPF). Picha|Mtandao.


  • Utekelezaji wake unakwamishwa na kutokuwepo kwa usawa, athari za utandawazi na mabadiliko ya teknolojia.
  • Tanzania kuwasilisha leo ripoti ya mapitio ya utekelezaji wa malengo hayo.
  •  UN, Antonio Guterres ametaka uwekezaji wa umma na sekta binafsi kwa ajili ya SDGs.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikitazamiwa kuwasilisha leo ripoti ya mapitio ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s), Umoja wa Mataifa (UN) umesema kutokuwepo kwa usawa, athari za utandawazi na mabadiliko ya teknolojia yanakwamisha nchi nyingi kupata maendeleo endelevu. 

Akizungumza jana (Julai 15, 2019) jijini New York, Marekani ambako Tanzania itawasilisha ripoti yake katika ufunguzi wa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la mawaziri (HLPF), Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres  amesema kuwa ikiwa ni miaka minne sasa tangu kupitishwa kwa ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030, bado juhudi za utekelezaji wake haziridhishi.

Amesema kwa mfano umasikini unapungua lakini sio kwa kiwango cha kutosha kutimiza lengo la kuutokomeza ifikapo 2030.

“Ongezeko la kutokuwepo usawa kunazuia ukuaji endelevu, sanjari na athari za utandawazi na mabadiliko ya teknolojia. 

“Tunashuhudia leo hii jinsi gani pengo la usawa linavyochochea changamoto za kiuchumi, kuondoa imani ya umma na kuathiri mshikamano wa kijamii, haki za binadamu na mafanikio,” alinukuliwa Guterres katika jukwaa hilo. 


Soma zaidi: Mipango endelevu inavyoweza kuipa uhai miradi ya umemejua Tanzania


Amebainisha pengo la usawa baina ya nchi na nchi ni kubwa, ingawa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua lakini kiwango cha mishahara kimedumaa huku asilimia 30 ya wasichana na asimilia 13 ya wavulana hawana elimu, ajira au ujuzi wowote. 

“Hakuna nchi yoyote duniani iliyo katika mtari unaotakiwa kufikia usawa wa kijinsia ifikapo 2030, na wanawake wanaendelea kuathirika na sheria za kibaguzi, pengo la usawa wa fursa na ulinzi, viwango vikubwa vya ukatili na hulka na mila potofu,” amesema. 

Hata hivyo, amesema kuna mengi ya kufanya kugeuza hali hiyo ikiwemo kuongeza uwekezaji wa umma na sekta binafsi kwa ajili ya SDGs, kushirikiana na kuongeza msaada wa nchi zilizoendelea kwa maskini na kutengeneza mfumo wa ufadhili wa afya ya kimataifa. 

Pia amesema kuwe na mazingira bora kwa sekta binafsi kuendelea na kuwekeza, kuhamia kwenye uchumi wa kijani kushughulikia suala la uhamiaji na kumaliza migogoro ya kisiasa duniani.