July 8, 2024

Safari ya mwisho ya Ephraim Kibonde kuhitimishwa jumamosi

Atapumzishwa katika makaburi ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam Machi 9, 2019.

  • Mwili wa marehemu utawasili leo usiku katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na utahifadhiwa katika hospitali ya Lugalo.
  • Shughuli za kuaga na mazishi zitafanyika Machi 9, 2019 katika makaburi ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Dar es salaam. Safari ya mwisho ya mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde aliyefariki leo katika hospitali ya Bugando mkoani Mwanza itahitimishwa jumamosi (Machi 9, 2019) katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.  

Mwili wa marehemu Kibonde unatarajiwa kuingia leo usiku ukitokea Mwanza na utapokelewa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) ili kuendelea na taratibu zingine za mazishi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group (CMG), Joseph Kusaga aliyekuwa akizungumza leo (Machi 7, 2019) kupitia Clouds TV, amesema kifo cha mtangazaji wao ni pigo lingine wakati bado wanaomboleza kifo cha Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Rugemalila Mutahaba aliyefariki hivi karibuni.   

“Clouds imepata pigo lingine kubwa kwa kumpoteza mtangazaji wake mahiri Ephraim Kibonde 12:30 ndiyo mwezetu Ephraim alipoteza maisha yake, nilipigwa simu saa moja na kufahamishwa kwamba Kibonde leo hamko naye tena,“ amesama Kusaga.


Inayohusiana: Clouds Media yapata pigo jingine, yampoteza Ephraim Kibonde


Akizungumzia taarifa za kifo cha Kibonde, Kusaga amesema marehemu alipata tatizo la kiafya ghafla akiwa katika msiba wa Ruge na alipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera kwa ajili ya matibabu akisaidia na mfanyakazi mwenzake Dk Isaack Maro.

Kutokana na hali yake, waliamua kumuamishia katika hospitali ya Uhuru ya jijini Mwanza na wakati akipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Buganda kwa matibabu zaidi, umauti ulimkuta njiani. 

“Tuliondoka Bukoba 2:30 nafikiri kuelekea Mwanza ambapo alipokelewa katika hospitali ya Uhuru pamoja na Dk Derick na Dk Isaack wakaangaika kumstabilize (kumuimarisha) baada ya hapa aliendelea vizuri.” amesema Kusaga na kuongeza lakini hali yake ilibadilika jana jioni (Machi 6, 2019) wakati wakijiandaa kurejea Jijni Dar es Salaam.

Marehemu Ephraim Kibonde siku za uhai wake akiwa studio za Clouds FM. Picha|Mtandao.

Baba asimulia mwanzo, mwisho wa Kibonde

Baba wa marehemu, Samson Kibonde amesema mtoto wake alianza kuumwa akiwa Bukoba kwenye mazishi ya Ruge ambapo aliongea naye siku ya jumanne na madaktari wakasema anaendelea vizuri.

“Mpaka jana wakasema wanatarajia labda angeweza kurudi leo asubuhi aletwe hospitali ya Dar es Salaam lakini usiku wa leo hali ikawa mbaya ikabidi ahamishiwe hospitali ya rufaa ya Bugando, madaktari wamejitahidi sana kushughulikia hilo,” amesema Samson Kibonde na kuongeza;

“Taarifa waliyotuletea kuwa hawajafaulu kwa sababu kulikuwa na uvimbe tumboni sasa baadaye walipojaribu kushughulikia jambo hilo, alfrajiri ya leo majira ya 10:00 tunaambiwa hali ilikuwa mbaya zaidi na saa 12:00 kamili mauti ikamfika mtoto wetu Efrahimu Kibonde.”

Mwili wa marehemu utawasili leo saa 4:00 usiku uwanja wa ndege na utapelekwa katika hospitali ya Lugalo kwa ajili ya kuhifadhiwa na ijumaa taratibu za maombelezo na mazishi zitafanyika nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na ofisi za Clouds Plus. 

Marehemu ataagwa rasmi na kupumzishwa jumamosi katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni.