July 5, 2024

Safari ya mwisho ya Mkapa ilivyohitimishwa kijijini Lupaso

Viongozi wataka Watanzania waendeleze mazuri yote aliyoyafanya wakati wa uhai wake.

  • Aagwa na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mtwara.
  • Apigiwa mizinga 21 na kupata heshima ya jeshi.
  • Viongozi wataka Watanzania waendeleze mazuri yote aliyoyafanya wakati wa uhai wake. 

Dar es Salaam. Ameimaliza safari yake  ya miaka 81 ya kuishi duniani. Sasa amepumzika katika nyumba yake milele baada ya kuimaliza kazi ya kuwatumikia Watanzania. Amelala na hatoamka tena. 

Huyo ni Mzee Benjamin Mkapa, ambaye leo Julai 29, 2020 majira ya saa 9 alasiri mwili wake ulihifadhiwa katika kaburi lilipo pembeni ya makaburi mengine yaliyopo katika nyumba ya familia ya Mkapa katika kjiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Safari ya Mzee Mkapa, aliyefariki  jijini Dar es Salaam Julai 23 mwaka huu baada ya kupata mshtuko wa moyo,  itahitimisha maombolezo ya siku saba yaliyotangazwa na Serikali ikiwa ni hatua ya kuenzi mchango wake katika maendeleo ya Tanzania. 

Watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais John Magufuli wamejitokeza kwa wingi leo kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Mkapa huku wakiwa na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao.

Safari ya mwisho ya Mkapa kuhitimishwa katika kijiji chake alichozaliwa ilikuwa si bahati mbaya kwa sababu kabla ya umauti kumfika alipenda azikwe huko. 

“Wakati Serikali ikipanga mahali pa maziko ya viongozi na tulipangiwa kuwa tunazikwa Dodoma kwa sababu ndiyo makao makuu, miaka miwili mitatu Mzee Mkapa akaniuliza mlipanga maziko yawe Dodoma? Mimi msinizike Dodoma, mimi Lupaso,” amesema Rais Magufuli wakati akitoa salamu kwa waombolezaji kabla ya kuzikwa kwa Mkapa. 

Rais Magufuli akiongea kwa unyenyekevu amesema “alitaka kuzikwa mahali alipozaliwa katika kijiji cha Lupaso.” 

Jeneza la Mzee Mkapa kabla ya kupumzishishwa katika nyumba yake ya milele leo kijijini kwake Lupaso mkoani Mtwara. Picha|Swahili Times. 

Apigiwa mizinga 21

Safari yake ya mwisho iliyohudhuriwa na maelfu ya watu wekiwemo wakazi wa Mtwara ilisindikizwa na gwaride la taratibu la wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWT) ambao walibeba mwili wa marehemu na kuuweka katika kaburi aliloandaliwa.

Viongozi na ndugu walipata fursa ya kuweka mashada ya maua juu ya kaburi baada ya kufunikwa. Mizinga 21 imepigwa angani ikiwa ni heshima za mwisho kwa kiongozi huyo aliyetawala Tanzania kati ya mwaka 1995 na 2005. 

Na hiyo ndiyo ikawa safari ya mwisho ya mzee wa “Ukweli na Uwazi”.


Zinazohusiana:



Viongozi watoa ujumbe mzito 

Rais Magufuli amesema jambo pekee ambalo Watanzania wanapaswa kumuenzi ni kuendeleza upendo aliokuwa nao hasa kwa wananchi wake, jambo lilimfanya kuwajali na kuhakikisha maisha yao yanaboreshwa. 

“Tujifunze kwa upendo mkubwa ambao ameuonyesha kwa wananchi wake,” amesema Rais John Magufuli.Akiongea kwa taratibu na unyenyekevu, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein amesema tunu aliyoiacha Mzee Mkapa ni kuimarisha Muungano wa Tanzania na waliobaki wanatakiwa kumuenzi kwa hilo.

“Aliyahifadhi na kuyatunza mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa vitendo. Alihifadhi na kuutunza Muungano wa Tanzania. 

Tunamuheshimu kwa hali yake na uzalendo aliokuwa nao. Tutaendelea kumuenzi maisha, tutamkumbuka katika maisha yetu na kumuombea kwa mwenyezi Mungu,” amesema Rais Shein.Licha ya kuwa Mkapa ametangulia mbele ya haki, bado Serikali na Watanzania wana kazi ya kutimiza ndoto yake katika kuongeza kipato cha Mtanzania.

Rais John Magufuli pamoja na Marais Wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Dk Jakaya Kikwete wakiweka mashada katika kaburi la Hayati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa aliyezikwa leo Lupaso mkoani Mtwara. Picha|Swahili Times.

Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete amesema licha ya kuwa Hayati Mkapa aliasisi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, bado Tanzania ina kazi kubwa ya kutekeleza dira hiyo licha ya kuwa tayari tumefika uchumi wa kati.

“Tumeshifika kwenye uchumi wa kati lakini hatujafika kwenye lengo lile ambalo tulilolikusudia la Dola (za Marekani) 3,000 (Sh6.9 milioni) la pato la kila Mtanzania ifikapo mwaka 2025 lakini naamini tukimpa nafasi Magufuli tena, naamini atapata, tutafika kule,” amesema Kikwete. 

Amesema  kiongozi huyo aliwapenda wananchi wake na alichukizwa na hali ya umaskini na aliupa uchumi kipaumbele ili kuboresha hali za Watanzania wanyonge. 

“Alikuwa kiongozi mzuri, alikuwa na mapenzi na wananchi wa Tanzania. Alikuwa anachukia sana mazingira tuliyokuwa nayo ya nchi kuwa maskini, watu kuwa maskini,” amesema Kikwete.