November 24, 2024

Safari ya mwisho ya Rais Magufuli kuhitimishwa Chato Machi 25

Mwili wa Hayati Dk John Magufuli unatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele wilayani Chato katika Mkoa wa Geita Machi 25 mwaka huu.

  • Atazikwa wilayani Chato katika Mkoa wa Geita Machi 25 mwaka huu.
  • Ataagwa na wananchi na viongozi katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Geita. 
  • Alkifariki dunia Machi 17 mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Dar es Salaam. Mwili wa Hayati Dk John Magufuli unatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele wilayani Chato katika Mkoa wa Geita Machi 25 mwaka huu.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akitangaza ratiba ya mazishi ya Dk Magufuli leo Machi 19, 2021 wakati akihutubia Taifa baada ya kuapa katika Ikulu ya Magogoni mkoani Dar es Salaam, amesema Taifa litaendelea na maombolezo ya siku 21 na bendera zitapepea nusu mlingoti.

Mama Samia amesema safari ya mazishi ya Hayati Magufuli itaanza kesho Machi 20, 2021 ambapo mwili wake utatolewa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo mkoani Dar es Salaam na utapelekwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Peter lililopo Oysterbay kwa ajili ya ibada.

Baadaye mwili wa Dk Magufuli utapelekwa uwanja wa Mkapa kwa ajili ya kuagwa na viongozi mbalimbali. 

“Tarehe 21, wananchi wa Dar es Salaam wataaga mwili wa Hayati Dk John Magufuli na baadaye mwili utasafirishwa kuelekea Dodoma,” amesema Rais Samia.

Jijini Dodoma, mwili wa Magufuli utaagwa Machi 22 kuanzia saa tatu asubuhi ambapo Mama Samia ameitangaza siku hiyo kuwa ni siku ya mapumziko.

Machi 23, mwili wa Rais Magufuli utaagwa Jijini Mwanza na baadaye utasafirishwa kwenda Chato ambapo utaagwa na wanafamilia na wananchi wa wilaya hiyo na maeneo ya  jirani siku inayofuata ya Machi 24.

Safari ya Mwisho wa Rais Magufuli itahitimishwa Machi 25 baada ya ibada itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Chato ambapo siku hiyo pia itakuwa siku ya mapumziko.

Baada ya ibada hiyo, Rais atapumzishwa katika nyumba yake ya milele na kukamilisha miaka 61 ya kuishi duniani. 


Soma zaidi


Rais Samia amesema kutakuwa na vitabu vya rambirambi ambavyo vitatolewa nchi nzima katika ofisi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kote nchini na baadhi ya sehemu maalum nchini ukiwemo ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na Nyerere Square Jijini Dodoma.

Pia, vitabu hivyo vitakuwa katika balozi zote za Tanzania zilizopo nchi za nje ili kutoa fursa kwa watu kutoa salamu zao. 

“Hatuna budi ila kusema bwana ametoa bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” amesema Rais Samia wakati akihitimisha kusoma ratiba ya mazishi ya Magufuli.