November 24, 2024

Safaricom yamteua Afisa Mtendaji Mkuu wa muda

Ni Michael Joseph, aliyewahi kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo kati ya mwaka 2000 hadi 2010, anayechukua nafasi ya Bob Collymore aliyefariki Julai mosi.

  • Ni Michael Joseph, aliyewahi kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo kati ya mwaka 2000 hadi 2010.
  • Atashika wadhifa huo hadi bodi ya wakurugenzi ya kampuni hiyo itakampomtangaza mtendaji mkuu wa kudumu.
  • Joseph anashika nafasi iliyoachwa wazi na Bob Collymore aliyefariki dunia kwa saratani Julai mosi, 2019.

Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya huduma za simu nchini Kenya ya Safaricom PLC imemteua Michael Joseph kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa muda kufuatia kifo cha aliyekuwa Mtendaji Mkuu Robert ‘Bob’ Collymore Julai mosi mwaka huu.

Taarifa ya kampuni hiyo kwa vyombo vya habari inaeleza kuwa Joseph, ambaye pia ni mjumbe wa bodi hiyo iliyoketi jana katika mkutano maalum, atashika wadhifa huo mpya hadi pale atakapotangazwa kiongozi wa kudumu wa kampuni hiyo.

Joseph (67), aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo kati ya Julai 2000 hadi Novemba 2010, atakaimu nafasi hiyo kufuatia kifo cha Collymore kilichotokea jana nyumbani kwake jijini Nairobi.


Soma zaidi: Bosi wa Safaricom afariki kwa saratani Kenya


Collymore alifariki kwa saratani ya damu iliyomsumbua kwa takriban miaka miwili sasa.

“Bodi ina imani kuwa katika kipindi hiki cha mpito, Joseph ataongoza vyema kampuni na wafanyakazi,” imesema taarifa hiyo ya Safaricom iliyotolewa na Katibu wa Bodi, Kathryne Maundu.

Mbali na kuwa ni mjumbe wa bodi ya Safaricom, Joseph ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege la Kenya (KQ).