November 24, 2024

Samia asimulia kazi ya urais ilivyo ngumu

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekiri kuwa kazi ya urais ni ngumu lakini inakua rahisi kwa sababu urais ni taasisi ambayo inafanya kazi na watu wenye taaluma mbalimbali.

  • Asema kazi hiyo ina ugumu kama hukujiandaa.
  • Asema urais ni taasisi na ndipo urahisi wake ulipo.
  • Awataka Watanzania kumuunga mkono.

Mwanza. Rais  wa  Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekiri kuwa kazi ya urais ni ngumu lakini inakua rahisi kwa sababu urais ni taasisi ambayo inafanya kazi na watu wenye taaluma mbalimbali.

Ugumu wa kiti hicho unakuja kama mtu hakujiandaa kukikalia, amesema Rais Samia alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari jana Juni 29, 2021 Ikulu mkoani Dar es Salaam.

Amesema wakati anachukua fomu ya mgombea mwenza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa urais mwaka 2020  hakujua kama atakuja kupokea kiti hicho.

Wakati anainadi CCM katika kampeni za mwaka jana alijua tayari anaye kaka yake ambaye ni Hayati John Magufuli kuwa atashikilia usukani wa kuliongoza Taifa.

“Labda niwaambie bila kupepesa, kazi ya urais ni ngumu lakini kwa sababu  urais ni taasisi yenye vyombo kadhaa vinavyosaidia ndipo urahisi wake ulipo. Rais afanye kazi peke yake kama mnavyojua Serikali ina sekta kadhaa ambayo kila linalozuka linashughulikiwa,” alisema Samia.

Rais Samia aliapishwa Machi 19 mwaka huu kuwa rais wa sita wa Tanzania baada ya kifo cha Rais Magufuli. 

Anasema kwa siku anapokea mafaili 30 ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi na kutolewa uamuzi ambapo wakati mwingine hulazimika kuyashusha chini kwa wasaidizi wake ili wamsaidie.

Hata hivyo, amesema ataweza kulimudu jukumu hilo nyeti la kuongoza nchi huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wananchi kutimiza malengo ya kuinua uchumi na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Nilikuwa najua tumeahidi nini kwa wananchi, tumejipanga kuwatumikia wananchi lakini kulifanya kama wewe lina ugumu wake. Hata hivyo, ninawathibitishia kuwa ninaweza kwenda nalo, nina usaidizi wa taasisi zote lakini kwa ushirikiano wenu wanahabari kwa pamoja tutafika,” alisema.

Samia alieleza suala hiyo wakati alipoulizwa swali na mmoja wa wahariri kuwa anaionaje kazi ya urais na matarajio yake baada ya kupokea kijiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake, Hayati Magufuli.

Maneno ya Rais Samia yanafaanana na mtangulizi wake, Hayati Magufuli ambaye mara kadhaa katika hotuba zake alikuwa akisema kazi ya urais ni ngumu na anatamani aache.