November 24, 2024

Saratani inavyowatesa wakazi wa Kanda ya Ziwa

Mikoa ya Kanda ya Ziwa inatajwa kuongoza kuwa na wagonjwa wengi wa saratani kutokona na mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya kemikali ya zebaki na samaki wa moshi.

  • Wengi wao hugundua kama wana ugonjwa huo wakiwa katika hatua za mwisho.
  • Matumizi ya kemikali ya zebaki, samaki wa moshi ni chanzo cha saratani.
  • Wataalam washauri wananchi kuchukua tahadhari mapema. 

Mwanza. Kija Charles (53), mkazi wa kijiji cha Lugeye wilayani Magu katika Mkoa wa Mwanza, hawezi tena kufanya shughuli za kilimo kama ilivyokuwa awali. 

Afya yake si imara tena. Hawezi kufanya shughuli hizo za kujiingizia kipato baada ya madaktari kumshauri asifanye kazi ngumu ili kupata muda kurejea katika hali ya kawaida kutokana na kufanyiwa upasuaji na kuondolewa kizazi. 

Kija aliondolewa kizazi ikiwa ni hatua muhimu ya kuokoa maisha yake baada ya kuugua ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ambao uligunduliwa na madakatari katika hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure. 

Kutokana na kuhitaji matibabu zaidi, baadaye alihamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini humo ambapo alifanyiwa upasuaji. 

“Siwezi kufanya kazi ngumu tena, hata tendo la ndoa nimeambiwa nisishiriki kwa sasa,” Kija aliiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) hivi karibuni. 

Kija ambaye ni mke na mama wa watoto 11 ni miongoni mwa wanawake na wanaume wa Tanzania wanaoteswa na madhila ya saratani za aina mbalimbali ambazo zimekuwa zikigharimu afya na uchumi wa familia zao.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani wapatao 50,000 na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la asilimia 50 ya wagonjwa wapya wa saratani nchini. 

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia tafiti za saratani (IARC) zinaonyesha kuwa mwaka 2018 Tanzania ilikuwa na idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ni 14,028 sawa na asilimia 33.3 ya wagonjwa wote nchini.

Aliyekuwa Makamu wa Rais Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya mashine ya kisasa ya tiba ya saratani kwa mionzi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Maiselage wakati hafla ya uzinduzi wa Jengo na mashine za tiba ya saratani mwaka 2019. Picha| Ofisi ya Makamu wa Rais.

Ugonjwa huo ulivyoanza kutafuna afya yake

Kija alianza kuhisi dalili za ugonjwa huo mwanzoni mwa mwaka 2016 baada ya kubaini mabadiliko kwenye mwili wake hasa katika kupata hedhi kila mwezi. 

“Mwanzoni nilijua ni hali ya kawaida kwa wanawake kupata siku zao za mwezi, lakini mabadiliko yalianza taratibu ambapo kwa mwezi likuwa napata hedhi kwa zaidi ya siku 10 na wakati mwingine mwezi mzima,” anasema mama huyo. 

Kwa mujibu wa Kija hakupata nafasi ya kwenda hospitali badala yake alijua ni mambo ya kawaida kwa kuwa katika kipindi hicho alikuwa anatumia dawa za kupanga uzazi.

Anasema aliamini huenda dawa hizo ndizo zinavuruga mzunguko wake wa hedhi na ndio chanzo cha yeye kupata hedhi mfululizo na baadaye alikatiza matumizi yake. 

Licha ya kuachana na  matumzi ya dawa hizo na kupata ushauri wa madakatari lakini hali ya kutokwa damu sehemu za siri iliendelea siku hadi siku.

Kwa kawaida mwanamke hupata hedhi kati ya siku 3 hadi 5 kwa mwezi. 

Mwaka 2019 mabadiliko zaidi yalijitokeza baada ya kugundua  ana uvimbe sehemu zake za siri na hakuwa na uwezo tena wa kushiriki tendo la ndoa mpaka sasa. 

“Mme wangu amenivumilia sana na hakuonyesha dalili yoyote ya kunitenga na kutoka nje ya ndoa,” anasema mama huyo kwa sauti ya unyonge.  

Kwa sasa, anasema bado yupo kwenye matazamio hali inayomfanya kuwa tegemezi  hadi hapo maelekezo ya watalaam wa afya  yatakapoamuliwa.


Soma zaidi: 


Ni nini kinasababisha saratani?

Daktari mbobezi wa magonjwa ya saratani kutoka hospitali ya rufaa Bugando, Bernad Ngombagira anasema saratani inasababishwa na mgawanyiko wa seli za mwili bila mpangilio.

Anasema kwa mtu mzima anakadiriwa kuwa seli trilioni 37 kwenye kila kiungo cha mwili 

Inapotokea seli hizo zinazaliana mfululizo bila kusimama au seli hizo hazifi zina uwezo wa kusambaa kwenda kwenye maeneo mengine ya mwili.

Kutokana na tatizo hilo, wataalamu wanasema husababisha kuwepo kwa ugonjwa wa saratani ambao umegawanyika katika makundi mawili ambapo moja ni saratani inayosababisha uvimbe na aina ya pili ni ile ya kimiminika ambazo zinakuwa saratani za damu.

Zipo aina nyingine  za saratani zaidi ya 200 zinatokea kulingana na mazingira, anasema. 

Kwa mujibu wa taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), saratani zinazoongoza ni saratani ya mlango wa shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake huku wanaume wakikabiliwa na saratani ya tezi dume sanjari na kibofu cha mkojo ambayo husababishwa na kichocho. 

Aina nyingine inayoripotiwa, Dk Ngombagira anasema ni saratani ya matezi, mfumo wa chakula na saratani ya ini.

Daktari mbobezi wa ugonjwa wa saratani kutoka hospitali ya rufaa ya Bugando, Dk Bernad  Ngombagira  wakati akizungumza na Nukta habari kuhusiana na ugonjwa huo. Picha| Mariam John.

Kwa mujibu wa Dk Ngombariga anasema kulingana na namna saratani inayojitokeza watu wazima kuanzia miaka ya 55 ndiyo waathirika zaidi wa ugonjwa huo huku watoto kuanzia miaka 12 nao huugua ugonjwa huu hususani saratani ya damu, tezi na figo 

“Karibia asilimia 50 ya wagonjwa wanaofikishwa katika hospitali hii kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wengi wanabainika kuwa na aina hizi za saratani,” anasema Dk Ngombariga. 

Kwa mwaka mmoja uliopita zaidi ya wagonjwa 15,000 wamepokelewa katika hospitali ya Bugando pekee huku wengi wakiwa katika hatua ya nne. 

“Wagonjwa wakiwa kwenye hatua hii ni nadra kutibika,” anasema daktari huyo.

Anasema asilimia 90 ya wagonjwa wa saratani au wagonjwa tisa kati ya 10 hufika hospitali wakiwa kwenye hatua ya tatu na ya nne ambapo robo tatu ya wagonjwa hao  hupoteza maisha. Ni robo au asilimia 25 ya wagonjwa wanaofika hapo, anasema, wanakuwa kwenye hatua ya kwanza na ya pili.

Usikose kufuatilia sehemu ya pili ya ripoti hii ambayo tutaangazia chanzo cha wagonjwa wengi wa saratani kutoka Kanda ya Ziwa, hatua za kugundua ugonjwa huo na mikakati ya Serikali kutokomeza saratani Tanzania.