October 6, 2024

Sekta tano za kuangaliwa kwa jicho la tatu bajeti ya Waziri Mkuu 2019-2020

Sekta hizo ni madini, uwekezaji, elimu, ajira na utalii ambazo zina mchanga mkubwa katika Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kila mwaka.

  • Sekta hizo ni madini, uwekezaji, elimu, ajira na utalii ambazo zina mchanga mkubwa katika Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kila mwaka. 
  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha yote iliyoahidi kufanya mwaka 2019/2020 yanatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.

Dar es Salaam. Wiki iliyopita April 4 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasilisha taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2018/2019 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020 ambayo imeangazia mambo mengi ikiwemo utekelezaji wa ahadi na mipango iliyopo kwa mwaka unaofuata. 

Taarifa hiyo pia inajumuisha makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020. 

Kwa mwaka 2019/2020, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake inatarajia kutumia Sh148.8 ambapo kati ya fedha, Sh86.3 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh62.5 ni za matumizi ya maendeleo. 

Katika taarifa hiyo, Majaliwa aliangazia mambo mengi yaliyofanywa na Serikali mwaka 2018/2019 na yale anayokusudia kufanya  mwaka 2019/2020. 

Nukta tunakuletea sekta tano muhimu za kuziangalia kwa jicho la tatu na mikakati iliyopo katika kuziboresha mwaka wa fedha unaofuata:

Uwekezaji

Majaliwa amesema kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji katika kujenga uchumi wa nchi, Serikali imeendelea kutoa uzito katika uwekezaji ambapo Rais John Magufuli, alichukua hatua ya kuhamishia masuala ya uwekezaji ikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kumteua Waziri wa Nchi, Angellah Kairuki kushughulikia masuala ya uwekezaji. 

Kutokana na jitihada hizo, hadi kufikia Februari, 2019 miradi mipya 145 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambapo inatarajia kuwekeza mitaji ya Dola za Marekani 1.84 bilioni na kuzalisha ajira mpya 15,491. 

Katika mwaka 2019/2020, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kutekeleza mapendekezo ya Mpango Kazi Jumuishi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini; kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji. 


Zinazohusiana:


Utalii

Katika hatua nyingine amesema sekta ya Utalii imeendelea kuimarika na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza ajira. 

Mathalan, idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2018 imeongezeka na kufikia watalii milioni 1.49 ikilinganishwa na watalii milioni 1.33 walioingia nchini mwaka 2017.

“Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.43 mwaka 2018 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 7.13,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Waziri Mkuu. 

Mwaka 2019/2020, Serikali imesema itaendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kuihamasisha na kuiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta hiyo kwa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga ili kuvutia watalii wengi zaidi nchini. 

Madini 

Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya madini na mchango wake katika kukuza uchumi, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya mabadiliko ya sheria ili kuhakisha inadhibiti rasilimali

Serikali imefanikiwa kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili namba 5 ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Mikataba ya Maliasili za Nchi namba 6 ya Mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura 123.

Majaliwa amebainisha kuwa Serikali inashughulikia kero zinazowakabili wachimbaji wadogo ili waweze kuendesha shughuli zao za uchimbaji mdogo na kunufaika na rasilimali ya madini.  

 Akitolea mfano mzuri wa utekelezaji wa dhamira hiyo ni Rais Magufuli kukutana na kufanya mazungumzo na wachimbaji wadogo Januari 2019, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao. 

“Vilevile, Mheshimiwa Rais alielekeza kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya zuio kwa wachimbaji wadogo maelekezo ambayo tayari yamefanyiwa kazi,” amesema Majaliwa. 

Hata hivyo, kibarua kilichopo mwaka 2019/2020 ni kukuza soko la ndani la madini kwa kuvutia wawekezaji na kuhamasisha shughuli za uongezaji wa thamani madini nchini. Pia, kuweka mkazo katika kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa masoko ya madini yenye ushindani mkubwa ili kudhibiti utoroshaji wa maliasili hiyo. 

Aidha, Serikali imebainisha kuwa itaendelea kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo, huduma za utafiti, teknolojia, mitaji na masoko. 

Matumizi ua mbinu za kienyeji katika uchenjuaji wa dhahabu yamekuwa yakiwanyima fursa wachimbaji wadogo kufaidika na madini hayo. Picha|Mtandao.

Elimu

Majaliwa amesema katika mwaka 2018/2019 Serikali tayari imetoa Sh166.44 bilioni hadi Februari, 2019 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa elimumsingi bila malipo nchini.

Imeboresha miundombinu ya shule za awali na msingi ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 6,521 kwa shule za msingi na hivyo kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa hadi kufikia 126,168 Februari 2019. 

“Kwa upande wa shule za Sekondari, vyumba 2,499 vya madarasa vimejengwa na kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 40,720 Mwaka 2018 hadi 43,219 kufikia Februari, 2019,” inasomeka sehemu ya ripoti ya Waziri Mkuu. 

Katika mwaka 2018/2019, Sh412.4 bilioni zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ambapo hatua hiyo, imeongeza idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo kufikia wanafunzi 119,214 kutoka wanafunzi 98,300 mwaka 2015.

Lakini katika mwaka 2019/2020, Majaliwa amezielekeza mamlaka zote zinazohusika na usimamizi na udhibiti wa ubora wa elimu zitekeleze majukumu yao ipasavyo kwa kutoa miongozo na kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuongeza ubora wa elimu inayotolewa. 

Uwekezaji katika miundombinu ya elimu nimuhimu kuwawezesha anafunzi kupata maarifa kuwawezesha kujibu mtihani. Picha|Mtandao.

Kazi, ajira na vijana

Katika kuhakikisha nguvukazi ya vijana inasaidia kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025, amesema katika mwaka 2018/2019, Serikali kupitia programu ya kuendeleza vijana imewezesha vikundi vya vijana 755 ambavyo vimepatiwa mikopo ya Sh4.2 bilioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuibua bunifu 31 za vijana katika sekta ya sayansi na teknolojia. 

Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kimitaji kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana, mapato ya ndani ya Halmashauri na programu ya kukuza ujuzi.

Katika kukuza ujuzi, vijana 32,563 wamewezeshwa kupata mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa ambapo mwaka 2019/2020 Serikali inakusudia kuwafikia vijana 46,950 katika fani mbalimbali zinatakazowasaidia kuajiriwa na stadi za kazi ikiwemo ufundi wa magari, useremala, uashi, upishi, huduma za vyakula na vinywaji, ufundi umeme, uchomeleaji, ufundi bomba, uchongaji vipuri na ushonaji nguo.

Kuhusu fursa za ajira, Majaliwa amesema hadi kufikia Februari 2019, ajira 221,807 zimezalishwa nchini ambapo zimetokana na utekelezaji wa miradi ya umma ya ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, ujenzi wa mji wa Serikali Jijini Dodoma, uimarishaji wa Shirika la Ndege Tanzania pamoja na ajira za moja kwa moja katika utumishi wa umma na uwekezaji katika sekta binafsi.

Kazi iliyopo mwaka 2019/2020 ni kushirikiana na wadau mbalimbali hususan waajiri na wafanyakazi, sekta binafsi, washirika wa maendeleo pamoja na vyama vya kiraia itaendelea kutekeleza programu zinazowezesha kuibua fursa zaidi za ajira.

Hata hivyo, Majaliwa hajaweka wazi katika kipindi hicho watatengeneza ajira kiasi gani na katika sekta zipi, jambo ambalo linazipa changamoto mamlaka husika katika kushughulikia tatizo la ajira nchini.