Sekta ya madini kinara utoroshaji mitaji Afrika
Takribani dola za Marekani bilioni 89 (Sh206.5 trilioni) hutoroshwa kutoka katika nchi za Afrika zaidi kupitia sekta ya madini.
- Takribani dola za Marekani bilioni 89 (Sh206.5 trilioni) hutoroshwa kutoka katika nchi za Afrika.
- Mitaji hutoroshwa zaidi kupitia sekta ya madini hasa ya dhahabu na almasi.
- Tanzania yapigiwa mfano kudhibiti wizi sekta ya madini.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNCTAD) imezitaka nchi za Afrika kuiga mfano wa Tanzania kwa kuanzisha vyombo vya ukaguzi katika sekta ya madini ili kudhibiti utoroshaji wa fedha na mitaji kwenda nje ya bara hilo.
Ripoti hiyo mpya kuhusu maendeleo ya uchumi wa Afrika ya mwaka 2020 iliyotolewa jijini Geneva, Uswisi Septemba 28, 2020 imesema kila mwaka, takribani dola za Marekani bilioni 89 (Sh206.5 trilioni) hutoroshwa katika nchi za Afrika na kulisababishia bara hilo umaskini na kukosa mitaji ya maendeleo.
Kiwango hicho kichotoroshwa ni sawa na asilimia 3.7 ya pato la ndani la Taifa barani humo.
UNCTAD katika ripoti hiyo inaeleza kuwa Afrika hupoteza fedha nyingi zaidi katika sekta ya madini kupitia utoroshwaji wa mitaji yake. Mwaka 2015 pekee dola za Marekani bilioni 15 (Sh34.7 trilioni) zilipotea, ripoti hiyo inabainisha.
Katika sekta ya madini, utoroshaji uliongoza katika mnyororo wa thamani wa madini ya dhahabu, almasi na platinamu.
Hata hivyo, ripoti hiyo imesema Tanzania imefanikiwa kudhibiti utoroshaji wa mitaji katika sekta ya madini kwa kuanzisha taasisi imara za ukaguzi ambazo zimesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato katika sekta hiyo.
“Serikali ya Tanzania imewekeza rasilimali kuongeza uwezo wa kukagua baada kushuhudia ukusanyaji mdogo wa mapato katika kipindi cha muongo mmoja wa uwekezaji wa sekta binafsi kwenye madini,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Soma zaidi:
- Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini
- Uzalishaji wa dhahabu Acacia washuka
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, taasisi kama hizo zikianzishwa katika nchi za Afrika zitasaidia kupunguza utoroshaji wa mitaji licha ya kuwa zinahitaji rasilimali za kutosha wakiwemo wafanyakazi waliobobea katika taaluma ya kodi, mazingira, tehama na madini.
UNCTAD inabainisha kuwa utoroshaji haramu wa fedha au mali kuwa ni kitendo cha mali au fedha zisizo halali au zilizopatikana kinyume cha sheria kuhamishwa kutoka sehemu moja au nyingine kwa ajili ya matumizi yasiyo halali.
“Utoroshaji wa fedha na mali unapora bara la Afrika na watu wake matumaini yao na unakwamisha uwazi na uwajibikaji huku vikimomonyoa imani kwa taasisi za Afrika,” amesema Katibu Mkuu wa UNCTAD, Mukhisa Kituyi wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.
Kituyi amesema uhamishaji wa mitaji unaweza kutokea pia kwa ukwepaji wa kodi au makadirio ya chini ya malipo ya kodi ya bidhaa zinazosafirishwa kwa meli, masoko haramu ya bidhaa, ufisadi na wizi.