October 6, 2024

Sekta ya manunuzi kuboresha mfumo wa utoaji taarifa kwa umma

Imebainika kuwa mfumo wa manunuzi uliopo sasa unakabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa taarifa.

  • Imebainika kuwa mfumo wa manunuzi uliopo sasa unakabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa taarifa. 
  • Watakiwa kuongeza elimu kwa wazabauni na wafanyakazi wa mashirika ya umma wanaotumia mifumo hiyo.

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kuboresha mfumo wa upatikanaji wa taarifa katika sekta ya manunuzi ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushindani wa zabuni zinazotangazwa kwa umma.

Hayo yamejiri katika warsha ya siku moja iliyowakutanisha Wataalam wa TEHAMA, wajasiriamali, wabunifu, wawakilishi kutoka Wakala wa Huduma ya Manunuzi Serikalini (GPSA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kujadili utendaji wa mfumo wa manunuzi katika taasisi za umma.

Wadau hao wamebainisha kuwa mfumo wa manunuzi uliopo sasa, hauwafikii watu wengi jambo linalopunguza ushindani wa zabuni na kupatikana kwa watu wenye uwezo na weledi wa kutekeleza mipango na miradi ya Serikali.

Tony Kirita kutoka shirika la Hivos Afrika Mashariki, amesema kuna kila haja ya kubuni mfumo mpya wa manunuzi jumuishi ambao unapatikana kwa urahisi mahali popote.  

“Tunaamini mawazo ya wengi, ndio chanzo cha mabadiliko,” amesema Kirita na kuongeza kuwa vijana wenye mawazo ya kibunifu wanaweza kuitumia fursa hiyo kutengeneza mfumo rahisi ambao utakuwa mwarobaini wa changamoto zilizopo katika sekta manunuzi.

Afisa Programu wa taasisi ya Tanzania Media Foundation (TMF), Vicencia Fuko amesema wakati mfumo mpya ukibuniwa ni vema uende sambamba na kuboresha upatinaji wa data na mikataba ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikivuruga manunuzi na kusababisha hasara kwa Taifa.

“Angalieni namna mnaweza kuja na njia za kuangalia mikataba na manunuzi ili kuleta uelewa kwa watu na jamii kwa ujumla,” Fuko.


Zinazohusiana: 


Baadhi ya wawakilishi kutoka katika mashirika ya umma wamesema mifumo iliyopo sasa bado sio rafiki kwa watumiaji hasa wanaotumia teknolojia ya kisasa ambapo mabadiliko hayo yatasaidia kuboresha huduma katika jamii.

“Changamoto bado ni ugumu wa upokeaji wa mabadiliko kwasababu wengi wamezoea mfumo wa mwanzo,” amesema Benard Ntelia, Meneja Usimamizi wa Mifumo ya TEHAMA kutoka  PPRA.

Ntelia amesema licha ya kuwepo kwa changamoto za mfumo wa utoaji taarifa bado unawanufaisha watu wengi na kinachotakiwa ni kuongeza elimu kwa wazabuni na wafanyakazi wa mashirika ya umma wanaotumia mifumo hiyo.

“Tunatumia mfumo wa TANePS ambao ulizinduliwa rasmi Juni 2017 na tuna imani watumiaji 25,000 watanufaika na mfumo huu,” amesema Ntelia.

Tony Kirita kutoka shirika la Hivos Afrika Mashariki akiwasilisha mada katika warsha ya siku moja ya wabunifu wa mifumo wa manunuzi. Picha| Zahara Tunda.

Mdau mwingine wa TEHAMA, Mussa Pepe amesema kuwa changamoto ya mashirika umma ni kutumia mfumo wake wa kukusanya taarifa hivyo kama wabunifu ni muda mzuri wa kubuni njia itakayowasaidia watu kuingia katika mfumo wa pamoja wa manunuzi.

“Nafikiri tubuni mfumo rahisi utakaowasaidia watu kuona manunuzi na tenda na kuwapa watu taarifa wakiwa katika eneo husika,” amesema.

Shirikala Budeshi nchini Nigeria limefanikiwa kubuni njia ya kuunganisha data za manunuzi na bajeti ili kuwasaidia wadau kufuatilia kwa undani manunuzi mbalimbali yanayofanyika katika masharika ya umma na binafsi.

“Kupatikana kwa habari kwa wadau kupitia ubunifu mzuri wa kiteknolojia, itatusaidia kupatikana kwa wazabuni wengi na itaongeza fursa za kiuchumi,” amesema David Nganila, Meneja sehemu ya Ununuzi, kutoka  Wakala wa huduma ya Manunuzi Serikalini (GPSA).

Hata hivyo, Shirika la HIvos linatarajia kuzindua mashindano ya wabunifu wa TEHAMA katika sekta ya manunuzi ya umma ikiwa ni njia ya kuongeza uwajibikaji na uwazi nchini.