Serikali ilivyojipanga kuwaokoa watoto wa mtaani
Katika kuhakikisha inapunguza idadi ya watoto wa mtaani, Serikali imesema inatekeleza mpango wa kuunganisha watoto na familia zao na kuwatafutia malezi mbadala wale wasio na familia.
- Inatekeleza programu ya kuwaunganisha na familia zao na kuwapatia malezi mbadala.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inapunguza idadi ya watoto wa mtaani, Serikali imesema inatekeleza mpango wa kuunganisha watoto na familia zao na kuwatafutia malezi mbadala wale wasio na familia.
Mpango huo umeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Mwanza tangu Novemba 2019 na utasamba katika mikoa yote yenye watoto wengi wa mtaani wanaoishi katika mazingira magumu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile akizungumza mapema Bungeni leo (Januari 28, 2020) amesema katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2019, waligundua watoto wa mitaani wanaoishi katika mazingira magumu 36,548 wakiwemo watoto wa kiume 17,894.