October 6, 2024

Serikali kutopanga bei ya pamba licha ya uzalishaji kushuka 2020

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga asema wataliachia soko liweze kuamua bei na Serikali kubaki kuwa msimamizi.

  • Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga asema wataliachia soko liweze kuamua bei na Serikali kubaki kuwa msimamizi.
  • Uzalishaji pamba unatarajiwa kushuka hadi tani 150,000 toka tani 348,000 msimu wa 2019 kutokana na mvua kuwa nyingi na kuathiri uzalishaji.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imejivua katika upangaji bei ya pamba baada ya Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga kueleza kuwa katika msimu wa mwaka 2020 hawatopanga bei ya zao hilo kwa wakulima ili kuwezesha nguvu ya soko kuamua na mkulima kupata soko la uhakika.

Mbali na kutangaza uamuzi huo, imesema kuwa inatarajia kuwa uzalishaji wa pamba nchini utashuka mara mbili katika msimu wa mwaka 2020 kutoka kiwango cha msimu uliopita.

Waziri Hasunga amewaambia wadau wa zao hilo Jumapili hii (Juni 7, 2020) kuwa Serikali itakuwa msimamizi mkuu kuhakikisha maslahi ya wakulima wa pamba yanalindwa muda wote.

“Kazi ya serikali ni kuweka mazingira wezeshi ya biashara ya zao la pamba kufanyika kama ilivyo kwa mazao mengine.Hivyo leo hapa hatutapanga bei badala yake tunaachia soko liamue,” amesema Hasunga katika taarifa iliyotumwa na wizara hiyo.

Pamba ni moja ya mazao makuu ya biashara Tanzania sanjari na kahawa, chai, tumbaku na korosho yanayochangia kuingiza fedha za kigeni. 

Kwa mujibu wa Kitabu cha hali ya uchumi mwaka 2018, pamba ilichangia kuingiza Dola za Marekani 68.38 milioni sawa na Sh157.2 bilioni.


Zinazohusiana:


Serikali hupanga bei elekezi katika baadhi ya mazao nchini ili kuhakikisha wakulimwa hawanyonywi na walanguzi ikiwemo korosho.

Dhamira ya Serikali, kwa mujibu wa Hasunga, ni kufanya Kilimo cha Tanzania kuwa cha kibiashara na si cha kujikimu kwa kuondoa zaidi vikwazo kwa wakulima.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha pamba yote ya wakulima inaongezwa thamani nchini kwa kutumia viwanda vya ndani na kuwataka wafanyabiashara wengi kujitokeza kununua pamba yote ya wakulima.

“Nitashangaa kuona mzalendo wa Tanzania akinunua pamba kwa bei ndogo na kuwanyonya wakulima,” amesema Hasunga katika kikao hicho kilichoshirikisha kuwashirikisha pia wakuu wa mikoa 17 inayolima pamba nchini.

Kuhusu kiwango cha uzalishaji katika msimu unaotarajia mwezi, Hasunga amesema wanatarajia kitashuka kutokana na uwepo wa mvua nyingi msimu huu, upungufu wa madawa na viuatilifu kwa baadhi ya wakulima.

” Tathmini ya awali imeonesha msimu huu uzalishaji pamba utashuka hadi tani 150,000 toka tani 348,000 msimu wa 2019 kutokana na mvua kuwa nyingi na kuathiri uzalishaji nchini,” amesema Hasunga.

Hasunga amewafahamisha wadau kuwa katika msimu uliopita wakulima nchini walipata zaidi ya Sh 419 bilioni zilizotokana na mauzo ya pamba ya takribani tani 348,000 iliyozalishwa nchini mwaka 2019.

Msimu wa ununuzi wa pamba mwaka 2020 unatarajiwa kuanza Juni 15.

Mwakilishi wa wanunuzi wa zao la pamba Christopher Gachuma amesema wamejipanga kuanza ununuzi wa pamba yote ya wakulima kwa kuzingatia bei ya soko.

Gachuma ameshukuru serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwahakikishia wanunuzi kuwa fedha zipo kwa ajili ya taasisi za fedha kukopa ili kununua pamba ya wakulima nchini