Serikali kutumia theluthi mbili ya bajeti nishati kugharamia mradi wa umeme Rufiji
Waziri wa nishati amesema Serikali itatekeleza mradi huo wa megawati 2,115 bila kuyumbishwa wala kukwamishwa na yeyote.
- Waziri wa nishati amesema Serikali itatekeleza mradi wa umeme wa maporomoko ya maji wa megawati 2,115 bila kuyumbishwa wala kukwamishwa na yeyote.
- Serikali itatumia Sh1.443 trilioni katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili kutekeleza mradi huo utaokamilika mwaka 2022.
Dar es Salaam. Serikali imepanga kutumia fedha za ndani Sh1.443 trilioni kutekeleza ujenzi wa mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji wa Megawati 2,115 ikiwa ni theluthi mbili ya bajeti yote ya wizara ya nishati kwa mwaka 2019/20.
Katika mwaka huo wa fedha unaoanza Julai 2019, Serikali imepanga kutumia Sh2.142 trilioni kwa ajili ya wizara ya nishati ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.6 kutoka bajeti ya mwaka huu unaomalizika Juni ya Sh1.692 trilioni.
Waziri wa Nishati Dr Medard Kalemani ameliambia Bunge leo kuwa Sh2.116 trilioni au sawa na asilimia 98.8 ya bajeti yote ya nishati ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku kiasi kilichosalia kikitumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
“Kati ya fedha hizo za maendeleo, Sh1.956 trilioni ni fedha za ndani na Sh160.08 bilioni ni fedha za nje,” amesema Dk Kalemani.
Sehemu kubwa ya fedha za maendeleo katika mwaka ujao wa fedha zitatumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme ya Mto Rufiji maarufu kama Stiegler’s Gorge Hydropower dam, mradi wa kimkakati wa kusambaza nishati vijijini na upanuzi wa mradi wa umeme wa gesi asilia wa Kinyerezi I wa megawati 185. Miradi hiyo mitatu kwa pamoja itagharimu Sh1.86 trilioni.
Soma zaidi:
Dk Kalemani amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa umeme wa Mto Rufiji katika mwaka wa fedha ujao ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuanza ujenzi wa bwawa (main dam and spillways); kuanza ujenzi wa njia za kupitisha maji (tunnels); na kukamilisha ujenzi wa njia ya pili ya umeme msongo wa kV 33 kutoka Gongo la Mboto.
“Fedha za ndani Shilingi trilioni 1.443 zimetengwa katika mwaka 2019/20 kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo. Utekelezaji wa mradi umeanza mwezi Desemba, 2018 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022,” amesema Dk Kalemani.
Kiwango hicho cha fedha kwa ajili ya kugharamia mradi huo wa umeme wa maji wa Mto Rufiji ni asilimia 67.3 ya bajeti yote ya wizara ya nishati katika mwaka wa fedha ujao.
“Kwa ujumla Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza mradi huu bila kuyumbishwa, kucheleweshwa wala kukwamishwa na mtu yeyote kutoka ndani au nje ya nchi asiyeitakia mema nchi yetu,” ameongeza.
Mradi wa Mto Rufiji, unaogharimu Sh6.5 trilioni, umekuwa ukipingwa vikali na baadhi ya watetezi wa mazingira ulimwenguni kuwa utekelezaji wake katika Pori la Akiba la Selous utasababisha uharibifu wa mazingira ikiwemo msitu na wanyama wa eneo hilo.
Hata hivyo, Desemba mwaka jana Rais John Magufuli alieleza kuwa mradi huo una faida nyingi kwa mazingira kuliko inavyodaiwa na watetezi hao wa mazingira ulimwenguni.
Dk Magufuli alieleza kuwa mradi huo utakapokamilika utasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kuwa watu watakuwa na uhakika wa kupata nishati ya umeme ya kupikia.