October 6, 2024

Serikali kuvipiga tafu viwanda vya pareto

Imesema inaangalia namna ya kuvisaidia viwanda hivyo kupata malighafi za ndani ili kuongeza uzalishaji.

Pareto ni zao la biashara lakini uzalishaji wake umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, teknolojia dunia na mabadiliko ya soko la ndani na nje. Picha|Mtandao.


  • Imesema inaangalia namna ya kuvisaidia viwanda hivyo kupata malighafi za ndani ili kuongeza uzalishaji.
  • Hatua hiyo itasaidia wakulima wa zao hilo kupata bei nzuri.
  • Itachochea ukuaji wa viwanda vya ndani ambayo imekuwa ni lengo la Serikali tangu mwaka 2015. 

Dar es Salaam. Serikali imesema inaangalia namna ya kuvisaidia viwanda vya pareto katika upatikanaji wa malighafi ya uhakika ili viendelee kuzalisha bidhaa bora na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo nchini. 

Kumekuwepo na madai kuwa wakulima wanauza maua ya pareto kwa walanguzi ambao wanasafirisha nje ya nchi ili kuepuka bei ndogo wanayoipata kutoka katika viwanda vya ndani. 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya aliyekua akizungumza bungeni leo (Mei 16, 2019) wakati wa kipindi cha maswali na majibu, amesema wameanza kufanyia kazi suala hilo katika baadhi ya viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini. 

“Kwa hiyo sisi tunafikiria kama Serikali tuna wajibu wa kuingilia kati kuona kwamba viwanda viweze kupata malighafi hizo kwa kusaidiwa na Serikali lakini mkulima aweze kupata bei inayostahili kutokana na kazi aliyoifanya,” amesema Mhandisi Manyanya.

Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mafinga mjini, Cosato Chumi aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani kudhibiti walanguzi ambao wanasababisha kiwanda cha pareto cha Mafinga kukokosa malighafi ya maua ya zao hilo. 

Cosato amebainisha kuwa ili Tanzania iwe na uchumi wa viwanda lazima tuhakikishe viwanda hivyo vinapata malighafi ipasavyo lakini kumekuwa na walanguzi ambao wananunua maua ya pareto na kuyasafirisha nje ya nchi na kusababisha kiwanda hicho kukosa malighafi.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Mhandisi Manyanya amesema changamoto inayopatikana katika kiwanda cha pareto Mafinga, pia iko katika maeneo mengine ambayo huhitaji malighafi nchini vikiwemo viwanda vya ngozi. 

“Changamoto ni kwamba kiwanda kinahitaji kipate hizo malighafi lakini utakuta baadhi ya viwanda vinanunua malighafi kwa bei ndogo kiasi kwamba mkulima anakuwa hapendi kupeleka hiyo malighafi katika kiwanda kama hicho,” amesema na kuongeza kuwa, 

“Lakini wakati huo huo hivyo viwanda vinahitaji malighafi hiyo kwa bei ndogo labda kutokana na uwezo wake mdogo wa kifedha hasa katika hatua za awali za ujenzi wa kiwanda.”

Amesema kutokana kuibuka kwa changamoto ya upatikanaji wa malighafi, Serikali imeanza kuingilia kati ili kuvisaidia viwanda vikiwemo vya pareto ili kuvihakikishia upatikanaji wa malighafi za ndani kuendeleza shughuli zao.


Zinahusiana: 


Zao la pareto huzalishwa katika mikoa ya Mbeya na Iringa ambapo baada ya kuvunwa maua yake husafirishwa hadi katika kiwanda cha kusindika pareto cha Mafinga (PCT). 

Pareto ni zao la biashara lakini uzalishaji wake umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, teknolojia dunia na mabadiliko ya soko la ndani na nje. 

Zao hilo hutumika kutengenezea vipodozi, dawa mbalimbali za kuua wadudu lakini unga wa maua ya pareto hutumika katika uhifadhi wa nafaka kama mahindi na maharage.   

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibu bei ya zao hilo imeimarika na kuwanufaisha wakulima waliowekeza katika uzalishaji wa zao hilo. 

Mathalani, mwaka 2017, bei ya zao la pareto ilipanda kutoka kati ya Sh1,500 hadi Sh2,700 mwaka 2016 na kufikia Sh2,000 hadi Sh3,000 kwa kilo.