November 24, 2024

Serikali kuweka utaratibu mpya uondoaji mizigo bandarini

Utaratibu HUO mpya utawaruhusu wananchi kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia wakala wa forodha.

Utaratibu huo hautahusisha mizigo inayopitishwa hapa nchini kwenda nje ya nchi (Transit Cargo). Picha|Mtandao.


  • Serikali kupendekeza utaratibu mpya utakaowaruhusu wananchi kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia wakala wa forodha. 
  • Mamlaka ya Mapato Tanzania itaandaa utaratibu wenye kueleweka kwa urahisi ili wananchi kugomboa mzigo ya kwa bei nafuu.
  • Utaratibu huo unaweza kuathiri makampuni ya uwakala bandarini.

Dar es Salaam. Huenda wananchi ambao walikuwa wanachelewa kuchukua mizigo yao bandarini wakapata ahueni, baada ya Serikali kupendekeza utaratibu mpya utakaowaruhusu wananchi kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia wakala wa forodha. 

Pendekezo hilo limetangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango Bungeni wakati akiwasilisha bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2019/2020. 

Amesema kupitia utaratibu huo mpya wa kuondoa mizigo bandarini, wananchi wa kawaida wataruhusiwa kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia wakala wa forodha (Clearing and Forwarding Agents), utaratibu ambao unatumika sasa.  

Amesema mchakato wa kuandaa uratibu huo unaendelea ili kuhakikisha unakuwa na ufanisi na kuongeza kasi ya kuondoa mizgo katika bandari za Tanzania.  

“Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania itaandaa utaratibu wenye kueleweka kwa urahisi ili kuwawezesha Wananchi kugomboa mizigo yao kwa gharama nafuu zaidi na bila kuchelewa,” amesema Waziri Mpango.


Zinazohusiana:


Hata hivyo, utaratibu huo hautahusisha mizigo inayopitishwa hapa nchini kwenda nje ya nchi (Transit Cargo). 

Huenda, utaratibu huo utakapoanza kutumika unaweza kuathiri makampuni ya uwakala wa forodha kwa sababu idadi ya wateja wanaohudumiwa watapungua. 

Utaratibu uliopo sasa, mwagizaji anapopokea ‘bill of lading’ ya mzigo wake anatakiwa kutafuta wakala wa forodha na kumpatia nyaraka muhimu za mzigo ili akamilishe taratibu zilizopo za kuutoa mzigo bandarini. 

Mchakato huu umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya watu kuwa unatumia muda mrefu na unaongeza gharama za ziada za kutoa mzigo bandarini.