Serikali ya Tanzania yafunga vituo 74 vya kutibu corona
Waziri wa afya Ummy Mwalimu amefunga kituo cha 74 kilichokuwepo hospitali ya Lulanzi mjini Kibaha kati ya 85 vilivyokuwepo nchini.
- Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema pamoja na kwamba ugonjwa huo upo ukingoni bado jamii na watumishi wa afya hawapaswi kubweteka.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imefunga vituo 74 vya kuhudumia wagonjwa wa virusi vya corona kati ya 85 vilivyokuwa vimeandaliwa baada ya kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo kupungua.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amefunga kituo cha 74 Ijumaa (Julai 3, 2020) kilichokuwepo katika Hospitali ya Lulanzi na kukikabidhi kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha huku akiwataka wakazi wa mji huo kutohofia kwenda kupatiwa matibabu kama hospitali nyingine.
Wizara hiyo hiyo imesema kituo hicho cha Lulanzi kilikuwa ni moja ya vituo vikubwa nchini vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa virusi vya corona kikiwa nyuma ya Amana, Mloganzila na Temeke.
Mgonjwa wa mwisho katika kituo hicho kwa mujibu wa Ummy aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo Mei 26 mwaka huu.
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Magufuli aeleza sababu za kutoifunga Dar licha ya wagonjwa kuongezeka
- Tanzania kuondoa kodi, ushuru wa vifaa tiba vya Corona
“Tunashukuru mwenyezi mungu kuwa Ugonjwa wa corona unaelekea mwishoni mwishoni kutoweka Tanzania. Tulikuwa na kambi 85 lakini leo zimebaki 11 tu ikiwemo hospitali binafsi,” amesema Ummy.
Waziri huo amesema kuwa pamoja na kwamba ugonjwa huo upo ukingoni bado jamii na watumishi wa afya hawapaswi kubweteka kwa kuwa kuna wasiwasi wa kutokea wimbi la pili la ugonjwa huo.
“Tuendelee kuhamasisha kuhimiza masuala ya kujikinga dhidi ya virusi hivyo,” amesema Ummy.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania ina visa vya wagonjwa wa corona 509 na vifo 21.
Katikati ya Juni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alibainisha kuwa hadi Juni 15 Tanzania ilikuwa na wagonjwa 66 pekee wa corona katika mikoa 10 huku 16 ikiwa haina mgonjwa kabisa.