Serikali ya Tanzania yajidhatiti kuongeza kasi ya unywaji maziwa shuleni
Serikali imesema itaendelea kuboresha maslahi ya wafugaji ili kuongeza kasi ya Watanzania kuywaji wa maziwa hasa wanafunzi waliopo shuleni.
- Imesema itaendelea kuimarisha sekta ya mifugo na kujenga viwanda ili kuongeza uzalishaji wa maziwa.
- Watanzania wanakunywa wastani wa lita 47 za maziwa kwa mwaka, ikiwa ni pungufu mara nne kwa kiwango kilichopendekezwa cha lita 200.
Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuboresha maslahi ya wafugaji ili kuongeza kasi ya Watanzania kuywaji wa maziwa hasa wanafunzi waliopo shuleni.
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 25, 2019) kwenye maadhimisho ya siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Iringa, amesema unywaji maziwa shuleni siyo tu ni muhimu lakini pia inatoa msukumo wa kuboresha afya hususan za watoto shuleni.
“Katika kuhakikisha azma hiyo ya Serikali inafikiwa, nitoe rai kwa wafugaji nchini kuunda ushirika imara utakaowawezesha kupata huduma mbalimbali za mifugo na ushirika huo pia ulenge katika kuboresha uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa, upatikanaji wa masoko pamoja na kuongeza kiasi cha usindikaji viwandani,” amesema Majaliwa.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa jana, inaeleza watalaamu wa lishe wanashauri kuwa mtoto apate glasi moja ya maziwa katikati ya siku itakayompatia lishe ya kutosha hadi atakapomaliza masomo yake kwa siku hiyo.
“Kwa bahati mbaya hapa nchini, watoto wengi huondoka asubuhi kwenda shuleni bila kupata chakula chochote. Aidha, shuleni nako mara nyingi hawapati chakula na hivyo hukosa usikivu mzuri katika masomo yao,” amesema Majaliwa.
Soma zaidi:
- CHATI YA SIKU: Uzalishaji wa maziwa waongezeka Tanzania lakini mwenendo wa unywaji hauridhishi
- Waziri Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
Zaidi ya nchi 70 duniani ikiwemo Tanzania ziliadhimisha siku ya unywaji maziwa na tayari zilishaanzisha mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa watoto wao.
Lengo ni kuhakikisha mtoto anapata lishe kamili na anakuwa na usikivu mzuri katika masomo yake. Mtoto amelengwa kwa sababu ni kundi ambalo ni muhimu katika kujenga Taifa lililo bora na anatarajiwa kurithisha vema vizazi vijavyo.
Programu ya unywaji maziwa shuleni ilianza kutekelezwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Dar es Salaam na Njombe.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa shule 40 na wanafunzi 34,561 katika mikoa hiyo wamenufaika katika kunywa maziwa lita 631,860 ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ushirikiano na Serikali, wazazi, wafadhili mbalimbali na wasindikaji wa maziwa.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina nia ya dhati ya kufanya mpango huu uwe wa kitaifa kwa kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita bilioni 2.7 zinazozalishwa sasa kwa mwaka mpaka lita bilioni saba kwa mwaka ifikapo 2020.
Hali halisi ya uzalishaji wa maziwa nchini
Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), uzalishaji wa maziwa nchini uliongezeka hadi kufikia lita bilioni 2.40 ikilinganishwa na lita bilioni 2.09 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 15.
Licha ya Tanzania kuzalisha maziwa mengi kila mwaka kutokana na mifugo iliyopo, bado hali ya unywaji maziwa hairidhishi.
Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2018/19 ni inaeleza kuwa Watanzania wanakunywa wastani wa lita 47 za maziwa kwa mwaka, ikiwa ni pungufu mara nne kwa kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) cha lita 200 kwa mwaka.
Hali hii inatoa fursa kwa Serikali na wadau wa maziwa kuongeza juhudi za kutoa elimu na kuwahamasisha Watanzania kunywa maziwa ili kuboresha afya zao.
Maziwa yana umuhimu kwa mwili wa binadamu hasa watoto kwani husaidia katika kujenga misuli ya mwili, ukuaji wa ubongo na huwa kama dawa ya kutibu maradhi mbalimbali.