July 8, 2024

Serikali yaeleza sababu JKT kusitisha mafunzo ya kujitolea 2020-21

Serikali imesema iliamua kusitisha mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mwaka 2020/21 ili kufanya tathmini na kuangalia namna vijana wanaweza kupata mafunzo bora yatakayowasaidia kujiajiri na siyo kutegemea kuajiriwa.

  • Ni pamoja na kuipatia muda JKT kutathmini ufanisi wa mafunzo yaliyokuwa yakitolewa awali. 
  • Pia kufanya mawasiliano na taasisi zingine kuongeza muda wa mafunzo ya wahitimu wa kidato cha sita kuwa mwaka mmoja badala ya miezi mitatu.

Dar es Salaam. Serikali imesema iliamua kusitisha mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mwaka 2020/21 ili kufanya tathmini na kuangalia namna vijana wanaweza kupata mafunzo bora yatakayowasaidia kujiajiri na siyo kutegemea kuajiriwa.

Machi 19 mwaka huu, JKT ilisitisha kwa muda  mafunzo ya kujitolea mwaka 2020/21 yaliyotarajiwa kuanza robo ya kwanza ya mwaka huu lakini haikusema sababu za kusitisha mafunzo hayo. 

Kutokana na kusitishwa kwa mafunzo hayo, vijana wote waliochaguliwa kuripoti kwenye kambi za JKT kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo hayo waliamuliwa kurejea majumbani mpaka watakapotaarifiwa tena. 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa amesema sababu kuu ya kusitisha mafunzo hayo ni kufanya tathmini ya kina kuhusu uafanisi wa mafunzo hayo kwa vijana wanaopata kila mwaka.

“Tulisitisha mafunzo ili kutoa nafasi kwa JKT kutathmini mafunzo yaliyofanyika na kuandaa utaratibu wa kuwa na mitaala bora ya mafunzo ya vijana itakayowawezesha vijana hao kujitegemea wanavyomaliza mafunzo badala ya kutegemea kuajiriwa,” amesema Kwandikwa leo Machi 31, 2021 Bungeni jijini Dodoma. 


Soma zaidi:


Amesema pia wanatoa fursa kwa JKT kukamilisha mpango wa kuwawezesha vijana kupata mitaji wanapomaliza mafunzo hayo.  

Jambo hilo litahusisha taasisi zingine ikiwemo Baraza la Uwezeshwaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kazi na Vijana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi.

“JKT itaendelea kutoa elimu kwa umma na kwa vijana wanaojiunga na JKT kujitolea kuelewa kwamba lengo la mafunzo ni kuwawezesha waweze kujitegemee badala ya kutegemea ajira,” amesema Kwandikwa.

Aidha, amesema katika kipindi hicho cha tathmini JKT  itafanya mawasiliano na taasisi zingine kama Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kuandaa utaratibu wa kuongeza muda wa mafunzo kutoka  miezi mitatu hadi mwaka mmoja. 

Waziri huyo amesema hatua hiyo itasaidia kuchukua vijana wengi wanaomaliza kidato cha sita na kupunguza idadi ya wanaojitolea kwenye kambi za jeshi.