Serikali yaeleza sababu kusitisha ununuzi mazao ya wakulima
Imesitisha ununuzi kwa muda kwa sababu maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) yamejaa.
- Imesitisha ununuzi kwa muda kwa sababu maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) yamejaa.
- Pia inafanya tathmini ya madeni inayodaiwa na wakulima.
- Corona yachangia wakulima kukosa soko nje ya nchi.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imesitisha kwa muda ununuzi wa mazao ya wakulima kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kujaa na hivyo kushindwa kupokea mazao mapya.
Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 20, 2020) alipotembelea ujenzi wa vihenge vya NFRA katika Mkoa wa Rukwa, amesema kwa sasa NFRA haiwezi kununua mazao kutoka kwa wakulima kwa sababu haina sehemu ya kuhifadhi.
“Lakini la pili ambalo walisimama (kununua mazao) na sehemu nyingine wakaendelea kusimama, ni kutokana na maghala yamejaa, pa kuweka hakuna, ushahidi ni ninyi watu wa Laela (mji wa Sumbawanga), ndiyo maana nikataka kuhakikisha kwa kuingia ndani kwanza, nimekuta humo ndani kumejaa, pa kuweka hakuna,” amesema Mgumba.
Mgumba amesema pia wamesimama kununua mazao ili kufanya tathmini ya madeni ambayo NFRA inadaiwa na wakulima licha ya kuwa hadi kufikia Septemba 18, 2020 hakukua na mkulima anayeidai Serikali.
Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa Serikali haitaki kuwakopa wakulima wakitambua kuwa wakulima hao hivi sasa wanajiandaa na msimu mpya wa kilimo na hivyo wanahitaji fedha.
Soma zaidi:
- Kigoma kinara usajili wa mashamba Tanzania bara
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki
Kujaa kwa maghala ya NFRA kumechangiwa na wanunuzi kutoka nchi za jirani kufunga mipaka yao ili kujikinga na ugonjwa wa Corona, jambo lililowafanya wakulima wakose soko la nje na kubaki na mazao mengi.
“Kuyumba kwa soko ni sababu ya janga la ugonjwa wa Corona, ndiyo maana mnaona wanunuzi kutoka nchi jirani zinazotuzunguka, Rwanda, Kenya, Uganda, Congo DRC wamepungua sana mwaka huu na kama wakija ni wachache sana, kwa sababu huko kwao bado wamejifungia kutokana na athari ya ugonjwa wa Corona,” amesema Mgumba.
Hata hivyo, Mgumba amesema Serikali inafanyia kazi changamoto hizo kwa kupanua wigo wa ujenzi wa maghala na vihenge vipya vya kuhifadhia chakula ili kununua mazao kutoka kwa wakulima
Katika Mkoa wa Rukwa, ujenzi wa vihenge vitatu unaendelea ili kukamilisha idadi ya vihenge nane ambavyo vinahitajika.
Pia amewataka wakulima kutumia soko la ndani kuuza mazao katika mikoa mbalimbali yenye mahitaji ya chakula ili kujipatia kipato wakati wakisubiri hali ikae sawa katika nchi za jirani ikiwemo Rwanda, Kenya, Uganfa na Congo DRC.
Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Agosti 2020 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa akiba ya chakula katika maghala ya NFRA imeongezeka hadi tani 90,255 mwezi Julai 2020 kutoka tani 52,724.7 mwezi Juni mwaka huu.
Ongezeko hilo linatokana na kuimarika kwa uzalishaji na msimu wa mavuno mwaka 2019/20.