October 6, 2024

Serikali yaelezea bidhaa za Zanzibar kuwekewa vikwazo Tanzania bara

Yasema hakuna bidhaa kutoka Zanzibar zilizozuiliwa kuingia Tanzania bara bali kinachojitokeza ni changamoto za kisheria na kikanuni ambazo zina utaratibu wake wa kuzishughulikia.

  • Yasema hakuna bidhaa kutoka Zanzibar zilizoiliwa kuingia Tanzania bara.
  • Yabainisha kuwa kinachojitokeza ni changamoto za kisheria na kikanuni ambazo zina utaratibu wake wa kuzishughulikia.

Dar es Salaam. Serikali imesema hakuna bidhaa kutoka Zanzibar zilizozuiliwa kuingia Tanzania bara bali kinachojitokeza ni changamoto za kisheria na kikanuni ambazo zina utaratibu wake wa kuzishughulikia.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya aliyekuwa akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu leo (Januari 28, 2020) bungeni jijini Dodoma, amesema  kwa kuwa nchi yetu ni moja hatutegemei kuwepo kwa vikwazo kutoka upande mmoja wa Muungano kwenda upande mwingine. 

“Kinachojitokeza ni changamoto chache za kisheria, kanuni na taratibu ambazo hata hivyo zimemewekewa utaratibu mahususi wa kushughulikia,” amesema Waziri huyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Welezo Saada Mkuya. 

Katika swali lake, Mkuya alitaka kujua  nini kinachosababisha baadhi ya bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kupata vikwazo kuingia katika soko la Tanzania Bara. 

Mhandisi Manyanya amesema utaratibu wa kushughulikia changamoto hizo hufanyika kwa njia ya vikao kwa ushirikiano wa kisekta ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa mwongozo wa sekta za pande mbili za Muungano kujadili changamoto kwa njia ya vikao kuanzia ngazi ya wataalam, makatibu wakuu na mawaziri na kushauri mamlaka za maamuzi. 

“Chini ya utaratibu huo, sekta ya viwanda na biashara kwa nyakati tofauti imekuwa ikipokea na kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto za biashara zilizoibuliwa kutoka pande zote mbili za Muungano,” amesema Manyanya. 


Soma zaidi: 


Akitolea mfano wa baadhi ya bidhaa zilizowahi kushughulikiwa chini ya utaratibu huo, amesema ni pamoja na kuku, maziwa na bidhaa nyinginezo.  

Hata hivyo, Mhandisi Manyanya a memtaka Mbunge huyo kuwasiliana na Wizara ya Viwanda na Biashara na kuwasilisha malalamiko ya bidhaa zinazowekewa vikwazo kama zipo zishughulikiwe ili kuimarisha Muungano uliodumu tangu mwaka 1964.