November 24, 2024

Serikali yafafanua ongezeko la kodi bidhaa zinazoingia Tanzania

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa itaongeza zaidi viwango vya ushuru na kodi vinavyotumika sasa kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani na kuwawezesha wafanyabiashara kuuza bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.

Serikali imedhamiria kulinda viwanda vya ndani na iko mbioni kupeleka Bungeni muswada ambao utaweka mazingira rafiki kwa Watanzania kufanya biashara. Picha| chuttersnap on Unsplash


  • Bidhaa hizo zinaweza kutozwa zaidi kodi iliyopo sasa kulingana na umuhimu wa bidhaa ili kulinda viwanda vya ndani. 
  • Kwa sasa Serikali hutoza asilimia 10 kwa bidhaa ghafi na asilimia 25 kwa bidhaa zilizo tayari kutumiwa na walaji.
  • Serikali kupeleka muswada Bungeni kuwezesha wafanyabiashara kuuza bidhaa kimataifa.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa itaongeza zaidi viwango vya ushuru na kodi vinavyotumika sasa kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini  ili kulinda viwanda vya ndani na kuwawezesha wafanyabiashara kuuza bidhaa hizo ndani na nje ya nchi. 

Utaribu uliopo sasa ni kutoza kodi kwenye bidhaa zinazoingia nchini katika kiwango cha asilimia 10 kwa bidhaa ghafi na asilimia 25 kwa bidhaa zilizo tayari kutumiwa na walaji.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya amesema bidhaa zinazotoka nje ya nchi zinaweza kutozwa zaidi ya asilimia 25 kulingana na umuhimu wa bidhaa ili kulinda viwanda vya ndani. 

Ametolea mfano malumalu (tiles), ambapo utafiti uliofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ulipendekeza kiwango cha ushuru wa forodha zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kuongezwa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35.

“Dhumuni kuu la kuongeza ushuru huu ni kuongeza tofauti ya bei ili kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya bidhaa zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema Mhandisi Manyanya bungeni leo (Januari 29, 2020).

Manyanya alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kulinda viwanda na wafanyabiashara wa ndani ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025. 

“Kwa mfano katika mwaka 2018/2019 Serikali iliongeza kodi kwenye mafuta ya kupikia yanayoingizwa nchini na kuweka vibali na leseni za udhibiti na usimamizi kwa baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje nchi kama vile vibali vya kuagiza sukari, mitungi, mitumba na magunia au viroba vinavyotumika kufungashia bidhaa,” amesema Naibu Waziri huyo.

Pia Serikali imeendelea kuboresha vituo vya pamoja vya mipakani yaani “One Stop Border Post (OSBP)” katika maeneo ya kuingiza bidhaa nchini, kwa mujibu wa Manyanya udhibiti na ukaguzi umeimarishwa katika viwanja vya ndege ili kudhibiti bidhaa za magendo, hafifu na bandia kuingizwa nchini. 


Zinazohusina: 


Muswada wa kulinda wafanyabiashara kutua bungeni

Baada ya Mhandisi Manyanya kujibu swali hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisimama na kuweka msisitizo kuwa Serikali imedhamiria kulinda viwanda vya ndani na iko mbioni kupeleka Bungeni muswada ambao utaweka mazingira rafiki kwa Watanzania kufanya biashara.

Amesema muswada huo utawasaidia wafanyabiashara kufanya biashara katika eneo huru la kibiashara la Afrika na maeneo mengine duniani. 

“Makakati wa Serikali siyo tu kulinda viwanda vya ndani, lakini mkakati wa Serikali ni kusaidia viwanda vya ndani na wafanyabiashara waweze kufanya biashara katika soko la pamoja la Afrika na kimataifa,” amesema Bashungwa.

Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson, ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuongeza hamasa kwa wananchi kuzikubali na kuzitumia bidhaa za ndani ili zipate kibali cha kusafirishwa nje ya nchi.

“Ipo fursa ya kufanya biashara za kimataifa lakini ndani ya nchi kwa kuzingatia hivyo vigezo maana sisi wenyewe tunataka maeneo yetu yatumie bidhaa za nje maana yake hatuzitaki za ndani, sasa nje  zitauzikaje kama sisi wenyewe hatuzikubali?… Tuweke viwango vya juu hata sisi tuweze kutumia bidhaa hizo hizo,” amesema Ackson.