October 6, 2024

Serikali yafungua milango uwekezaji mapori yaliyopandishwa hadhi

Uwanja wa ndege wa Chato kuwa kiungo muhimu kwa watalii kufika eneo hilo.

  • Yataunganishwa na kuunda Hifadhi moja ya Taifa ili kuwanufaisha wananchi na Serikali.
  • Uwanja wa ndege wa Chato kuwa kiungo muhimu kwa watalii kufika eneo hilo.
  • Kumesheheni vivutio vingi likiwemo Ziwa Ngoma katika Pori la Akiba Kimisi

Dar es Salaam. Serikali imefungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika mapori matano ya akiba yaliyopandishwa hadhi yaliyopo mikoa ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Mapori hayo ni pamoja na Pori la Akiba la Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika ambapo Serikali inakusudia kuyaunganisha ili kuunda hifadhi moja ya Taifa.  

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Karagwe mkoa wa  Kagera, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema mapori hayo yana hazina kubwa ya vivutio vya utalii ambavyo vikutumiwa vizuri vitawanufaisha wananchi wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.

Uwekezaji unaohitajika katika mapori hayo ni ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya nyota moja hadi zenye nyota tano, nyumba za kulala wageni, uanzishwaji wa kampuni za utalii pamoja na kutoa huduma za vyakula kwa ajili ya  watalii.

Tayari Serikali imefuta kodi ya kuingiza magari ya watalii nchini  ili kuwawezesha wananchi na wawekezaji kuingia katika biashara hiyo ikiwa na lengo la kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta ya utalii.

Baadhi ya watalii wakishuhudia mandhari nzuri ya wanyama. Picha| mwananchi.co.tz

Pori la Akiba Burigi lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,941 limepakana na wilaya za Karagwe, Muleba na Ngara mkoani Kagera, wakati Kimisi likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,030 katika wilaya za Ngara na Karagwe mkoani humo.

Biharamulo lina ukubwa wa kilomita za mraba 731 katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita,  Ibanda likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 200 na  Rumanyika kilomita za mraba 800 katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

Mapori haya yapo katika eneo muhimu la kukuza soko la watalii kutoka ukanda wa Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato na reli ya kisasa (Standard Gauge Railway) itakuwa muhimu katika kutoa mawasiliano.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ndio yalikuwa yanasimamia mapori hayo na , sasa yatakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Kwa mujibu wa Hasunga mapori hayo matano yana hazina kubwa ya vivutio vya utalii likiwemo ziwa Ngoma lililopo kwenye pori la akiba Kimisi.