Serikali yafuta maonyesho ya nane nane mwaka 2021
Fedha zilizotengwa kwa ajili shughuli hiyo zitatumika kuimarisha huduma za ugani ili kuleta mapinduzi ya kilimo.
- Sherehe hizo zilizokuwa zifanyike mwezi Agosti, 2021 katika kanda nane katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
- Fedha zilizotengwa kwa ajili shughuli hiyo zitatumika kuimarisha huduma za ugani ili kuleta mapinduzi ya kilimo.
- Serikali kufanya tathmini ya ufanisi ya maonyesho hayo miaka ijayo.
Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda ametangaza kufutwa kwa sherehe za maonyesho ya wakulima maarufu kama Nane Nane kwa mwaka 2021 na fedha zilizotengwa kwa ajili shughuli hiyo zitatumika kuimarisha sekta ya kilimo.
Sherehe hizo zilitakuwa zifanyike mwezi Agosti, 2021 katika kanda nane katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Prof Mkenda amesema Serikali inakusudia fedha zote za umma zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe hizo zitumike kuimarisha huduma za ugani nchini.
“Shughuli zote za Nanenane mwaka huu zimefutwa rasmi na Serikali. Hhivyo fedha zote zilizotengwa kwa kazi hiyo zitatumika kuboresha huduma za ugani nchini ili kuleta mapinduzi ya kilimo,” amesema waziri huyo leo (Februari 10, 2021) Jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari.
Amesema shughuli za Nane Nane lazima ziendane na upatikanaji wa huduma bora za ugani kuinua sekta ya kilimo, hivyo Serikali lazima ijipange vema.
Zinahusiana:
- Kigoma kinara usajili wa mashamba Tanzania bara
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki
Kufuatia uamuzi huo wa Serikali, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau itatumia muda huo kufanya tathmini ya namna maonyesho ya Nane Nane yamekuwa yakifanyika na kuona maeneo ya kuboresha ili yawe na tija katika kukuza sekta ya kilimo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, Prof Mkenda amesema wizara yake itaunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kufanya tathmini hiyo ili kilete mapendekezo yatakayokuwa na tija katika maadhimisho ya Nane Nane katika miaka ijayo.