July 5, 2024

Serikali yakerwa vivuko vya majini kukosa vyoo

Ni kivuko kilichopo kijiji cha Ilunda wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza ambacho hakina huduma muhimu.

  • Ni baada ya Naibu Waziri Mwita kutembelea  kivuko cha Ilunda mkoani Mwanza.
  • Kivuko hicho hakina vyoo, ofisi za wakata tiketi na jengo la abiria. 
  • Aagiza vivuko vyote nchini vifanyiwe maboresho.

Mwanza. Serikali imetoa siku 14 kwa wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) kuhakikisha inafanya marekebisho ya changamoto kwenye vivuko vyote vya majini nchini ikiwa ni pamoja na kujenga vyoo, ofisi za wakata tiketi na majengo la abiria. 

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi kwenye kivuko kilichopo kijiji cha Ilunda wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza na kubaini hakina maeneo hayo muhimu.

Naibu Waziri huyo akiwa ameongozana na timu ya wataalam kutoka Temesa, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Seny’i Nganga  pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo, Hamis Tabasamu amemwagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi kumwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Tamesa nchini kuhakikisha wanafanya tathimini kwenye maeneo hayo na kufanyia marekebisho haraka.

Amesema katika ziara yake aliyoifanya nchi nzima amekutana na changamoto hizo za ukosefu wa sehemu hizo maalum ambapo abiria hulazimika kujisaidia vichakani.

“Ukienda nchi zingine vivuko vya Serikali vinaheshimika kwa kuwa mazingira yake yameboreshwa lakini kwa hapa hali siyo, vivuko vingi havina vyoo, jengo la abiria na la kukatia tiketi, pamoja na maegesho,” amesema Waitara.

Amesema hawawezi kupeleka mabilioni ya fedha kwenye vivuko na wasiweze kujenga choo. 

“Nimewagiza Katibu Mkuu wa ujenzi afanya mapitio ya vivuko vyote nchi nzima na afanye tathimini ya kujenga,” amesema Waitara.

Awali baadhi ya wananchi walimweleza Waitara kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa choo kwenye kivuko hicho na hivyo kusababisha kujisaidia vichakani, jambo linalotishia afya zao.

“Hatuna choo tunalazimika kujisaidia mlimani tunaomba Serikali itujengee choo ili kutuepushia magonjwa ya mulipuko kama kuhara na kipundupindu,” amesema  Fadhili Abdallah mkazi wa kijiji cha Ilunda

Kwa upande wake Meneja wa Tamesa  Kanda ya Ziwa, Hassan Kalonda amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kumweleza naibu waziri huyo kuwa watalishughulikia suala hilo.

Kalonda amesema zaidi ya Sh800 milioni zimetengwa kwa ajili ya kufanyia marekebisho vivuko 10 kikiwemo cha Ilunda.

Mbunge wa jimbo hilo, Hamisi Tabasamu amesema pamoja na changamoto hizo kuwepo lakini pia kivuko kinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara hali inayosababisha kujiendesha kwa hasara.

Amesema kivuko hicho kinachofanya safari kati ya Kijiji cha Ilunda wilayani Sengerema na Luchelele wilayani Nyamagana kwa mwezi hukusanya zaidi ya Sh4.5 milioni huku matumizi yake yakiwa ni zaidi ya Sh13 milioni.

Amesema tatizo linalosababisha hasara kwenye kivuko hicho ni kutokuwepo kwa barabara itakayosaidia magari kupita kuvusha mizigo kwenda ng’ambo ya pili ambayo ni kilomita 24.

Naibu Waziri aliahidi kutatua changamoto zilizoainishwa na mbunge huyo kuwa atahakikisha barabara inatengenezwa.