Serikali yapendekeza kufuta msamaha wa kodi taulo za kike
Waziri wa fedha na mipango amesema msamaha huo umeshindwa kuwanufaisha walengwa na badala yake wafanyabiashara walitumia fursa ya kujiongezea faida.
- Waziri wa fedha amesema msamaha huo umeshindwa kuwanufaisha walengwa na badala yake wafanyabiashara walitumia fursa ya kujiongezea faida.
- Uamuzi huo wa Serikali ni pigo kwa watoto wa kike na kina mama ambao walitarajiwa kunufaika na msamaha wa kodi hiyo.
Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya kuweka msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye tauli za Kike maarufu kama pedi, Serikali inapendekeza kuondoa msamaha kwa maelezo kuwa haukuwasaidia walengwa kama ilivyotarajiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango amelieleza Bunge leo wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2019/20 kuwa msamaha huo haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha wafanyabiashara.
“Aidha, wakati Serikali ilipoweka msamaha huu ilitarajia kwamba wazalishaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi,” amesema Dk Mpango.
Hatua hiyo ya Serikali huenda ikapingwa zaidi na wanaharakati nchini kutokana na msukumo wa muda mrefu uliokuwepo katika kuondoa kodi hiyo ili kuwawezesha watoto wa kike waweze kujisitiri vyema wakati wakiwa katika siku zao za hedhi.
Mapema mwaka Mbunge wa Viti (Chadema) Maalum Upendo Peneza na wanaharakati wengine walivalia njuga kuondolewa kwa VAT katika taulo hizo ambazo ni muhimu kwa afya za wasichana na kina mama.
Uamuzi wa Serikali kuweka msamaha katika taulo hizo ulipokelewa kwa shangwe na wadau mbalimbali nchini kuwa utawawezesha watoto wa Kike kununua bidhaa hizo.
Hadi sasa mpira umebaki kwa wabunge iwapo watapitisha pendekezo hilo Serikali ama la.
Taulo za kike hutumika na watoto wa kike na kina mama katika kujisitiri katika siku zao za hedhi. Serikali inapendekeza kuondoa msamaha wa VAT katika bidhaa hizo. Picha|Mtandao.