November 24, 2024

Serikali yasema fedha za kigeni kununua bidhaa nje ya nchi inaridhisha

Amesema kiasi cha fedha hizo ni Dola za Marekani bilioni 4.39 hadi kufikia Aprili, 2019, kuiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma nje ya nchi kwa takriban miezi 4.3.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema nchi ina fedha za kigeni za kutosha kununua bidhaa na huduma. Picha|MCL Digital.


  • Amesema kiasi cha fedha hizo ni Dola za Marekani bilioni 4.39 hadi kufikia Aprili, 2019.
  • Zitawezesha kununua bidhaa na huduma nje ya nchi kwa takriban miezi 4.3 juu ya ukomo unaotakiwa.
  • Amesema zinaongeza imani kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hadi kufikia Aprili 2019 akiba za fedha kigeni ilifikia Dola za Marekani bilioni 4.39 kuiwezesha nchi kuendelea kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi 4.3.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza bungeni leo (Juni 13, 2019)  wakati wa uwasilishaji wa hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2019/2020, amesema akiba hiyo ya fedha za kigeni ni ya kuridhisha na kukidhi mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi. 

“Akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani bilioni 4.39 Aprili 2019 kiasi ambacho kinatosha kuagiza huduma na bidhaa nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi 4.3.

“Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuridhisha na kukidhi mahitaji ya kuagiza bidhaa nje ya nchi na pia kuongeza imani kwa wawekezaji katika uchumi,” amesema Dk Mpango.


Soma zaidi: 


Amesema kiasi hicho kinaongeza imani kwa wawekezaji ambao wanawakeza katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na kuwepo kwa hali nzuri ya uchumi. 

Amebainisha kuwa kiwango hicho cha akiba ya fedha za kigeni ni zaidi ya lengo la nchi la kuwa na akiba ya kutosha ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda miezi 4.0.  

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017, akiba ya fedha za kigeni iliongezeka hadi kufikia dola za Marekani milioni 5,906.2 mwezi Desemba 2017 ikilinganishwa na dola milioni 4,325.6 Desemba 2016 ambapo kiasi hicho kilikuwa na uwezo wa kulipia bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 5.4.