July 8, 2024

Serikali yatoa ahueni tano kwa wafanyabiashara 2019-2020

Inakusudia kufanya maboresho ya mfumo na sera ili kufuta na kupunguza baadhi ya kodi, ushuru na tozo.

Ahueni nyingine iliyopendekezwa na  Serikali ni kuanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko ya taarifa za kodi dhidi ya TRA. Picha|Mtandao.


  • Inakusudia kufanya maboresho ya mfumo na sera ili kufuta na kupunguza baadhi ya kodi, ushuru na tozo. 
  • Wafanyabiashara kuwekewa kitengo huru cha kutoa malalamiko ya kodi.
  • Kuanzishwa kwa dawati la kushughulikia mapingamizi ya makadirio ya kodi.

Dar es Salaam. Huenda wafanyabiashara wakapata ahueni ya kodi na mazingira ya biashara zao yakaboreshwa, baada ya Serikali kuainisha mikakati mbalimbali ya mfumo na sera inayokusudia kutekeleza katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 unaoanza julai mwaka huu. 

Mikakati hiyo imewekwa katika hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 iliyowasilishwa Bungeni Juni 13, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ambapo amesema Serikali itaanza kutekeleza mpango unaolenga kuwapa nafuu wanyabiashara hapa nchini.

“Napenda niwahakikishie wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itaanza kutekeleza kwa nguvu zaidi mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint for the Regulatory Reforms to improve the Business Environment) ili mazingira ya biashara nchini yawe rafiki zaidi na yenye gharama nafuu,”amesema Dk Mpango. 

Serikali inapendekeza kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni (Corporate Income Tax) kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2019/20 hadi mwaka 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike.

Serikali itasaini mkataba wa makubaliano na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo likiwa kuwavutia wawekezaji katika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali. 

Pia Serikali inapendekeza kutoa msamaha wa kutengeneza hesabu za makampuni  zinazotakiwa  kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya ukokotoaji wa Kodi ya mapato kutoka kiwango cha sasa cha Sh20 milioni hadi Sh100. 

“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa mlipa kodi ya kutafuta mtaalam (Certified Public Acountant) kwa ajili ya kutengeneza hesabu,”amesema Dk Mpango.


Zinazohusiana: 


Aidha, kutokana na  malalamiko ya walipa kodi kuhusu ukadiriaji wa kodi na uthaminishaji wa bidhaa usio na uhalisia, Serikali inapendekeza TRA kuanzisha dawati la kushughulikia mapingamizi ya makadirio ya kodi ambapo pingamizi la uthamanishaji na utambuzi litashughulikiwa ndani ya saa 24.

Wafanyabiashara watapewa nafuu ya kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). 

Hatua hii inatofautiana na hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN anaanza kufanyiwa tathmini (tax assessment) ya mapato yake ya biashara na kutakiwa kulipa kodi. 

‘’Hatua hii itawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wapya kupata muda wa kujiandaa na mahitaji yanayotakiwa katika shughuli wanazofanya na kuondoa usumbufu au dhana ya woga wakati wa kuanzisha biashara,” amesema Dk Mpango. 

Ahueni nyingine iliyopendekezwa na  Serikali ni kuanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko ya taarifa za kodi dhidi ya TRA

Dk Mpango amesema kitengo hicho kitasimamiwa na kuratibiwa na wizara yake ili kuhakikisha kinakuwa na ufanisi wa kushughulikia kero za wafanyabiashara.

“Kitengo hiki kitahusisha kupokea na kupitia malalamiko ya kodi zinazotolewa na walipa kodi au watu wenye nia njema,” amesema Dk Mpango.