July 8, 2024

Serikali yatoa mwelekeo mpya mpango wa maendeleo wa Taifa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wenye dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu wa Tanzania.

  • Imezindua Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wa 2021/22–2025/26.
  • Una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu wa Tanzania.
  • Watanzania watakiwa kushiriki kuutekeleza.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wenye dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu wa Tanzania.

 Mpango huo wa 2021/22–2025/26 utagharimu Sh114.8 trilioni ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Sh40.6 trilioni 40.6 na zilizobaki zitatoloewa na sekta ya umma. 

 “…fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wetu wa maendeleo. Kwa niaba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba fedha hizi zitapatikana na malengo tuliyojiwekea yatatekelezwa,” amesema Majaliwa. 

Waziri Mkuu ametoa hauli hiyo leo Juni 29, 2021 wakati akizindua mpango huo katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

                           

Waziri Mkuu amesema mpango huo una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi.

Pia utaisidia kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.

“Kamwe hatutafumbia macho tabia ya ukwepaji kodi, kazini, ufujaji wa fedha na rushwa na tutaendelea kuenzi bunifu na kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa mpango huu,” amesema Majaliwa. 

 Katika Mpango huo, miradi ya kielelezo itaendelea kutekelezwa kama ilivyokuwa katika mpango wa iili hususan ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115; ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta (EACOP) na ununuzi wa meli na ujenzi wa bandari ya uvuvi (Mbegani).

Amesema mpango huo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025; Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020; Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/12–2025/26 na Matokeo ya Tathmini Huru ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17–2020/21.

“Wizara ya Fedha na Mipango endeleeni na utaratibu wa kutoa elimu ya kutosha ili kumwezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu katika utekelezaji,” ameagiza mtendaji huyo mkuu wa Serikali.

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Christine Musisi amesema wananchi, Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi watautumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. 

 Pia ameihakikishia Serikali kwamba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yataunga mkono utekelezaji wa mpango huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.