November 24, 2024

Serikali yavuna gawio la Sh100 bilioni kampuni ya madini ya Twiga

Rais John Magufuli amesema fedha hizo zitatumika kuboresha huduma za jamii.

  • Katika kampuni hiyo, Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa. 
  • Rais John Magufuli amesema fedha hizo zitatumika kuboresha huduma za jamii. 
  • Stamico nayo yatoa gawio la Sh1.1 bilioni kwa Serikali. 

Dar es Salaam. Kampuni ya madini ya Twiga imetoa gawio la Dola za Marekani milioni 40 sawa na Sh100 bilioni kwa Serikali ya Tanzania ikiwa ni miongoni mwa makubaliano ya uanzishwaji wa kampuni hiyo. 

Kampuni hiyo (Twiga Minerals Corporation Limited) inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya madini ya Barrick Gold. 

Rais John Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Oktoba 13, 2020) katika hafla ya utoaji wa gawio hilo jijini Dar es Salaam, amesema gawio hilo ni sehemu ya makubaliano ya uanzishwaji wa kampuni hiyo ambayo Serikali inamiliki hisa za asilimia 16.

“Tulikubaliana faida ambayo itakuwa ikipatikana tutakuwa tugawana asilimia 50 kwa 50. Hii ndiyo sababu leo hii tuko hapa kushuhudia kampuni ya Twiga minerals ikitoa gawio la Dola za Marekani milioni 40 sawa na takriban Sh100 bilioni. 

Ameishukuru kampuni ya Barrick kukubali kufanya mazungumzo na Serikali yaliyochukua takriban miaka miwili ambayo sasa yameanza kuzaa matunda kwa Watanzania.  

Kampuni ya Madini ya Twiga inasimamia migodi mitatu ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu. 

Amesema gawio hilo litatumika katika utoaji na uboreshaji wa huduma za jamii na maisha ya Watanzania.

“Hizi fedha ambazo zimeingia kama gawio zitapeleka watoto wetu kusoma shule bure, tutanunua madawa, tutatengeneza barabara, tutatengeneza na kujenga hospitali zetu, tutasomesha la kwanza mpaka vyuo vikuu, tutatoa huduma za kila aina kwa Watanzania,” amesema Dk Magufuli.

Pia Rais Magufuli ameshuhudia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) likitoa gawio la Sh1.1 bilioni kwa Serikali ikiwa ni sehemu ya faida yake. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko gawio lilitolewa na kampuni ya Twiga ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini kwa miaka mitano iliyopita. 

Amesema kabla ya mwaka 2015 mapato yaliyokuwa yanatokana na madini yalikuwa hayazidi Sh115 bilioni kwa mwaka 2020, Serikali imefanikiwa kukusanya Sh528 bilioni.

“Kabla ukuta (wa Mererani) haujajengwa, mapato ya jumla ya Tanzanite yalikuwa kilo 312 zenye thamani ya Sh4.1 bilioni lakini leo tumeshazalisha kwa mwaka mmoja kilo 2.772 zenye thamani ya Sh30.75 bilioni,” amesema Biteko.