October 6, 2024

Serikali yawaonya wanaoingiza mafuta ya kupikia kimagendo

Wafanyabiashara watakaokiuka onyo hilo kuchukuliwa hatua kali za kisheria

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atoa maagizo mazito uagizaji mafuta ya kupikia. Picha| Vidokezo


  • Yazitaka mamlaka husika kudhibiti uingizwaji wa vyakula visivyokuwa na virutubisho.
  • Watakiwa kuzingatia Sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219.
  • Wafanyabiashara watakaokiuka onyo hilo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuhakikisha zinachukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika kuingiza nchini bidhaa za chakula na mafuta ya kupikia kwa njia za magendo.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Novemba 15, 2018) wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Vullu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni Jijini Dodoma.

Mbunge huyo amehoji kuhusiana na suala la uagizwaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje kama unazingatia sheria iliyopitishwa na Serikali ambayo inalazimisha vyakula na mafuta ya kula kuwekwa virutubisho.  

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, ipo sheria (Sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219) inayohusu udhibiti wa vyakula yakiwemo mafuta ya kupikia ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na imeweka utaratibu wa kudhibiti uzalishaji, uagizaji, usambazaji pamoja na uhifadhi wa mafuta.

“Sheria hiyo pia inataka vyakula vyote vikiwemo vile vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa hapa nchini yakiwemo mafuta ya kupikia, lazima viwekewe virutubisho. Wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kulinda afya ya mlaji,” amesema Majaliwa. 

Ameziagiza mamlaka husika kuhakikisha zinaendelea kudhibiti uingizwaji holela wa bidhaa mbalimbali za vyakula visivyokuwa na virutubisho yakiwemo mafuta ya kupikia na kutoa adhabu kali kwa wafanyabiashara watakaobainika kuingiza bidhaa hizo nchini.


 Zinazohusiana: 


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inakusudia kuanzisha kurugenzi au idara itakayosimamia fukwe zote nchini zikiwemo za bahari na maziwa  ili kuziimarisha na kuzifanya ziwe miongoni mwa vivutio vya utalii nchini.

Amesema kuimarishwa kwa fukwe hizo kutawezesha watalii kupata maeneo ya kupumzika mara wanapotoka kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivyopo nchini kama mlima Kilimanjaro pamoja na mbuga mbalimbali za wanyama.

Majaliwa alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Kiteto Zawadi Koshuma aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza utalii nchini kupitia fukwe zilizopo katika ukanda wa bahari na maziwa, ambazo  zimeachwa bila kuendelezwa.