October 7, 2024

Serikali yawatoa hofu wakulima wa pamba Tanzania

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakulima na kuwahakikishia kuwa pamba yao yote iliyopo gharani itanunuliwa katika kipindi kifupi kijacho.

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakulima na kuwahakikishia kuwa pamba yao yote iliyopo ghalani itanunuliwa katika kipindi kifupi kijacho
  • Ununuzi wa zao hilo umefikia asilimia 80 hadi Septema 10, 2019. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakulima na kuwahakikishia kuwa pamba yao yote iliyopo ghalani itanunuliwa katika kipindi kifupi kijacho.

Majaliwa ametoa hakika hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa aliyetaka kujua mustakabari wa zao hilo nchini kwenye kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu mapema leo Septemba 12, 2019.

“Wanunuzi wanakwenda kuchukua pamba. Tuna uhakika katika kipindi kijacho, pamba yote itatoka mikononi mwa wakulima na itabaki mikononi mwa wanunuzi ili utaratibu wa kwenda kufanya mauzo uendelee,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema Serikali imewashirikisha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kufuatilia kwa karibu zoezi la ununuzi wa pamba katika maeneo yote.

“Baada ya kuchanganua pamba iliyobaki kwa wakulima, tumeigawa  kwa wanunuzi maalumu ambao wana uhakika wa kuinunua pamba hiyo,” amesema Majaliwa.

Aidha, Majaliwa amesema hadi sasa, ununuzi wa pamba umefikia takribani asilimia 80 ambapo hadi kufikia Septemba 10, 2019, Serikali imenunua takribani tani 235,000 na pamba iliyobaki ni kidogo na itanunuliwa na wanunuzi. 


Zinazohusiana


Waziri Mkuu amesema uzalishaji wa zao la pamba nchini umeongezeka hadi kufikia tani 350,000 katika msimu wa 2018/2019 kutoka tani 220,000 mwaka 2017/2018.  

Ikumbukwe kuwa, pamba inategemewa zaidi na wakulima wa mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Tabora, Mara, Kagera, Singida, Kigoma na Katavi, ambapo ni miongoni mwa mazao saba ya biashara yanayoingizia Tanzania fedha nyingi za kigeni. 

Mathalani, mwaka 2017 pamba iliingiza fedha za kigeni Sh80.2 bilioni ikiwa juu kidogo ya katani iliyoingiza Sh57.7 bilioni na nyuma ya Chai.