July 8, 2024

Serikali yazibana kampuni zisizotoa ujuzi kwa wafanyakazi wazawa

Yawataka wageni waliojiriwa Tanzania kuhakikisha wanawarithisha wafanyakazi wazawa ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi zao vizuri baada ya wageni hao kumaliza muda wao wa kazi.

  • Ni zile zilizoshindwa kutekeleza mpango wa urithishaji ujuzi (Succession Plan) kwa wazawa.
  • Yawataka wageni waliojiriwa Tanzania kuhakikisha wanawarithisha wafanyakazi wazawa ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi zao vizuri baada ya wageni hao kuondoka nchini. 

Dar es Salaam. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Patrobas Katambi amewataka wageni waliojiriwa Tanzania kuhakikisha wanawarithisha wafanyakazi wazawa ujuzi utakaowasaidia kufanya kazi zao vizuri baada ya wageni hao kumaliza muda wao wa kazi. 

Amesema agizo hilo ni utekelezaji wa mpango wa urithishaji ujuzi (Succession Plan) kwa wafanyakazi wazawa kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Kuratibu Ajira kwa Wageni ya mwaka 2015. 

Akizungumza mara baada ya kuwasili kwenye mgodi wa Barrick mkoani Mara, Katambi amesema kuwa Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi ikiwemo suala la utoaji wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni ili kihakikisha vibali vinavyotolewa ni kwenye kada au ujuzi ambao ni adhimu katika soko la ndani la ajira. 

“Hivi sasa vibali vya kazi kwa raia wageni vimekuwa vikitolewa hususan kwa wenye ujuzi ambao ni adhimu, na wageni hao wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza mpango wa kurithisha ujuzi kwa wazawa ili waweze kutekeleza majukumu yao baada ya wageni hao kumaliza muda wao wa kazi hapa nchini,” amesema Katambi.


Soma zaidi: 


Utekelezaji wa mipango ya urithishaji ujuzi utasaidia kulinda ajira za wazawa kupitia ujuzi walionao raia wakigeni wanaofanya kazi hapa nchini na hivyo Watanzania wengi wataweza kuwajibika na kuimarisha utendaji wao utakuwa bora zaidi katika kada hizo ambazo zilikuwa zikisimamiwa na wageni hapo awali.

Amesema kumekuwa na wimbi kubwa la maombi ya wafanyakazi wa kigeni kwenye maeneo mbalimbali wakitaka kuleta raia wa kigeni ambao kazi zao zinaweza kufanywa na wazawa. 

“Yapo baadhi ya makampuni ambayo yamekuwa na tabia ya kutokurithisha ujuzi kwa wafanyakazi wazawa ili kukwamisha wazawa wasiweze kuendelea kufanya kazi ambazo zilikuwa zikifanywa na wageni hao lengo ikiwa kampuni hizo ziendelee kutegemea sana wageni kutoka nje ya nchi,” amesema Naibu waziri huyo, 

Amesema waajiri ambao watakashindwa kutekeleza mpango wa urithishaji ujuzi kwa wazawa watachukuliwa hatua stahiki za kisheria.