October 7, 2024

Sh700 milioni kujenga shule ya sekondari ya wasichana Lindi

Shule hiyo itajengwa katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi maalum kwa wasichana.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee wa kijiji cha Narungombe wilayani Ruangwa  baada ya kuzungumza na wananchi  kijijini hapo Juni 22, 2020. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Shule hiyo itajengwa Ruangwa mjini maalum kwa wasichana. 
  • Pia Shule ya Sekondari ya Liuguru inatarajiwa kujengewa mabweni na kubadilishwa kuwa ya wasichana.
  • Majaliwa amesema hiyo itawasaidia wasichana kupata elimu bora. 

Dar es Salaam. Serikali imetenga Sh700 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ili kuwawezesha kupata mazingira mazuri ya kusomea na kutimiza ndoto zao za elimu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania inataka mtoto wa kike asome kuanzia darasa la awali hadi elimu ya juu na kwamba ujenzi wa shule za wasichana utasaidia katika kuwaondolea vikwazo ambavyo vinasababisha washindwe kufikia malengo yao kielimu.

 “Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya elimu, wazazi mnatakiwa muhakikishe watoto wote wa kike na wa kiume wanakwenda shule. 

 “Na kuhusu elimu kwa mtoto wa kike tumeboresha na sheria kali imetungwa kwa watakaokatisha masomo yao,” amesema Waziri Mkuu leo Juni 22, 2020 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Chikwale, Nangurugai, Machang’anja, Narungombe na Liuguru wilayani Ruangwa.

Amesema mbali na ujenzi wa shule hiyo maalum ya sekondari ya wasichana ambayo itajengwa Ruangwa mjini, pia Shule ya Sekondari ya Liuguru inatarajiwa kujengewa mabweni na kubadilishwa kuwa ya wasichana.

 “Tayari Serikali imetoa Sh180 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na bwalo katika Shule ya Sekondari ya Liuguru ambayo tunataka iwe ya watoto wa kike ili wasome kwa utulivu bila kuguswa guswa na waweze kutimiza ndoto zao,” amesema Majaliwa. 


Zinazohusiana:


 Kuhusu watoto wa kiume waliokuwa wanasoma shule ya Sekondari ya Liuguru, Waziri Mkuu amesema watakwenda kusoma katika shule ya Sekondari ya Narungombe ambayo nayo itakuwa ya bweni kwa watoto wa kike na wa kiume na tayari Serikali imetoa Sh80 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bweni.

 Akizungumzia kuhusu kuporomoka kwa bei ya ufuta, Waziri Mkuu amesema inatokana na bei ya soko la dunia na kuwa hali hiyo itakoma kwa kujenga viwanda vya kuchakata mazao hayo nchini, 

 “Suala la bei ya mazao linapangwa na wanunuzi, Serikali inasimamia tu,” amesema huku akiwataka wakulima wawe watulivu wakati Serikali ikilifanyia kazi suala hilo.