Shirika la biashara duniani lapata bosi wa kwanza mwanamke
Ni Dk Ngozi Okonjo-Iweala ambaye ni mtaalam wa uchumi kutoka Nigeria. Ni mwanamke na Mwafrika wa kwanza kushikilia nafasi hiyo katika chombo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995.
- Ni Dk Ngozi Okonjo-Iweala ambaye ni mtaalam wa uchumi kutoka Nigeria.
- Dkt Okonjo-Iweala ni mwanamke na Mwafrika wa kwanza kushikilia nafasi hiyo katika chombo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995.
- Ataanza safari ya kutekeleza majukumu yake ifikapo Machimosi mwaka huu.
Dar es Salaam. Mtaalam wa uchumi kutoka Nigeria Dk Ngozi Okonjo-Iweala amechaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) na anakuwa mwanamke wa kwanza na Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kushika wadhifa wa juu katika shirika hilo tangu kuanzishwa kwake 1995.
Mwanamama huyo ambaye ni gwiji wa uchumi anatarajiwa kuanza majukumu yake ifikapo Machi mosi mwaka huu na atakua madarakani hadi Agosti 31, 2025.
“Huu ni wakati wa kipekee kwa WTO. Kwa niaba ya Baraza Kuu, natuma salamu zangu za pongezi kwa Dk Ngozi Okonjo-Iweala kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WTO na ninamkaribisha katika mkutano huu wa Baraza Kuu,” amesema Mwenyekiti wa Baraza la WTO David Walker katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika Februari 15, 2021..
Walker amemshukuru Dk Okonjo-Iweala kwa uvumilivu wake wakati wa miezi tisa ya uchaguzi huku akiweka wazi kutarajia ushirikiano kutoka kwa wanachama wa shirika hilo katika kipindi cha uongozi wake ili kusongesha mbele shughuli za WTO.
Dk Okonjo-Iweala anachukua nafasi ya mtangulizi wake Roberto Azevêdo aliyetangaza kuachia wadhifa huo mwaka mmoja kabla ya kumaliza kipindi chake.
Azevedo aliachia rasmi kiti hicho Agosti 31 mwaka jana.
Soma zaidi:
- Mfahamu mwanamke nguli anayehubiri teknolojia ya Blockchain Tanzania
- Hedhi: Ni fahari ya kuwa mwanamke
- “Ubongo wa mwanamke umechangamka zaidi kuliko wa mwanaume”
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, Dkt Okonjo-Iweala amesema kipaumbele chake kikuu ni kushirikiana na wanachama kushughulikia haraka athari za kiuchumi na kiafya zilizoletwa na janga la Corona au COVID-19.
“Ni heshima kubwa kuchaguliwa na wanachama kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WTO. WTO thabiti ni muhimu sana katika kujikwamua haraka na vyema kutoka katika mvurugano uliosababishwa na janga la COVID-19.
“Natarajia kushirikiana na wanachama kutekeleza sera za kuchukua hatua ili turejeshe tena uchumi wa dunia mahali pake.” amesema kigogo hiyo.
Kuteuliwa kwa mtaalam huyo wa uchumi kushika nafasi ya juu ya WTO ni muendelezo wa viongozi wa dunia kutambua uwezo na nafasi ya mwanamke kulete maendeleo duniani.
Miongoni mwa wanawake wanaoshika nafasi za juu ni Kristalina Georgieva kutoka Bolivia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) huku Kamala Harris akichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Marekani baada ya uchaguzi uliofanyika mwaka 2020.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed amempongeza Dk Okonjo-Iweala kwa nafasi aliyoipata kwa sababu ni hamasa kwa wanawake wote duniani kutimiza ndoto zao na kutoa mchango bora katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (DSG’s).
Warm congratulations to Ngozi Okonjo-Iweala—newly appointed Director-General of the @WTO.
You are blazing new trails as the first woman & first African to lead WTO. You inspire us. The @UN looks forward to working with you to keep the promise of the #SDGs for people & for planet pic.twitter.com/7TnmO4E7xh— Amina J Mohammed (@AminaJMohammed) February 15, 2021