November 24, 2024

Shirika la ndege la Emirates lachukua hatua dhidi ya virusi vya Corona

Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuboresha usafi kwa kutumia kemikali inayoua virusi vya Corona.

Ndege za Emirate zinasafishwa saa moja kabla ya kuanza safari. Picha| Emirates.


  • Shirika hilo la ndege limeongeza kiwango cha usafi kwa kuanza kutumia kemikali ya kuua virusi hivyo ndani ya ndege zake.
  • Wageni kutoka Thailand, China na Italia kupimwa wanapowasili Dubai.
  • Wasafiri ambao safari zao zimeahirishwa kurejeshewa fedha na kuomba nafasi kwa ajili ya safari mpya.

Dar es Salaam. Shirika la ndege Emirates la nchi za Falme za Kiarabu limeimarisha hali ya usafi kwenye ndege zake zote ikiwa ni hatua inayochukuliwa kuwakinga watumiaji wa ndege hizo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19) unaosambaa kwa kasi duniani. 

Emirates kupitia taarifa iliyotolewa leo (Machi 9, 2020) imesema pamoja na kuongeza kiwango cha usafi, shirika hilo limeahirisha safari zake katika nchi ambazo haziruhusu wageni kuondoka au kuingia kutoka katika  nchi ambazo zimeathirika na virusi hivyo.

“Shirika linatumia kemikali iliyothibitika kuua virusi na vimelea na kuhakikisha usalama wa abiria dhidi ya uchafu utokanao na muingiliano wa virusi, bakteria na fangasi ndani ya ndege ambayo ni rafiki kwa mazingira,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Usafi huo unaofanywa na watu takriban 36 kulingana na ukubwa wa ndege unafanywa saa moja kabla ya ndege kuanza safari yake.

Aidha, kwa nchi zao zimezuia safari, Shirika hilo limesema abiria walioathirika na zuio hilo wanaweza kupanga safari upya ambazo zitaanza Mei 31, 2020 huku msafiri akiwa na uwezo wa kushika nafasi yake kwenye ndege hizo au kubadili ruti yake hadi Juni 30 japo huduma hiyo itatolewa kwa baadhi ya maeneo tu.


Zinazohusiana


Kwa wateja ambao safari zao zimeahirishwa, wanaweza kupanga safari zingine zitakazoanza Machi 31, 2020  au kubadili ruti na kuomba nafasi nyingine ya kusafiri hadi Juni 31 mwaka huu.

Pia Shirika hilo limesema litarudisha fedha za tiketi ambazo hazijatumika au kutoa vocha za safari zenye gharama sawa na tiketi iliyokatwa.

Kwa upande wa jiji la Dubai la Falme za Kiarabu (UAE) , Shirika hilo limesema linachukua vipimo kwa wageni wote wanaotokea Jiji la Beijing (China), Beirut (Lebanon) na majiji ya Italia yakiwemo Roma, Venice, Bologna na Milan.

Nchi nyingine ambayo watu wake watapitia vipimo ni Thailand ambapo wageni kutoka miji ya Phuket na Bangkok watalazimika kufanyiwa vipimo.

Wasafiri wengine wanaopitia viwanja vya Dubai watapitia vipimo vya kubaini joto na kuendelea na safari zao.

Ugonjwa wa Corona ulilipuka nchini China mwishoni mwa Desemba 2019 ambapo mpaka sasa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi jana umeshaua 3809 huku watu zaidi 109,577 wakiambukizwa ulimwenguni. 

Hadi sasa, nchi ya China imeripoti asilimia ya 81.9 ya vifo huku kesi 80,904 zikitokea nchini humo.