October 7, 2024

Shirika la ndege la Emirates lawapa ahueni wafanyabiashara Dar

Limepunguza nauli kwa wasafiri wanaotumia ndege zake kutoka Dar es Salaam hadi Dubai.

Muonekano wa moja ya ndege za shirika la ndege la Emirates ambalo limejipatia umaarufu duniani. Picha|Mtandao.


  • Limepunguza nauli kwa wasafiri wanaotumia ndege zake kutoka Dar es Salaam hadi Dubai
  • Watakaosafiri kati ya Machi 26, 2019 hadi Septemba, 2019 watapata punguzo la bei ya kusafirisha mizigo.
  • Wafanyabiashara walita shirika hilo kuendelea ofa ili kuwapa fursa za kusafiri zaidi nje ya nchi. 

Dar es Salaam. Huenda wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafiri kwenda Dubai wakapata ahueni ya kupunguza gharama za usafirishaji bidhaa, baada ya shirika la ndege la Emirates kutangaza kushusha nauli kwa wasafiri wanaotumia ndege hizo. 

Emirates imefikia uamuzi huo Machi 26, 2019, ikiwa ni ofa maalum kwa wateja wake wa  jijini Dar es Salaam wanaosafiri kwenda Dubai kwa daraja la biashara na uchumi.

Katika taarifa yake, Emirates imeeleza kuwa lengo la ofa hiyo ni kuongeza safari za kutoka Tanzania hadi Dubai pamoja na kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika nchi hiyo lakini kwa wafanya biashara huenda ikawa ni njia mojawapo ya kupata ahueni ya usafirishaji mizigo.

Mtumiaji wa ndege za shirika hilo atakayesafiri kwa daraja la uchumi atalipa Dola za Marekani 489 (Sh1.124 milioni) na daraja la biashara ni Dola 1,499 (Sh3.447 milioni). 

Kwa mujibu wa shirika hilo, ofa hiyo ni kwa tiketi zilizokatwa kuanzia Machi 26, 2019 na Aprili 9, 2019 ambapo zinatakiwa zitumike kwa safari zilizoanza Machi 26 hadi Septemba 30 2019. 

Japo kuwa ofa ni ya muda mfupi, inaweza kuwanufaisha wafanya biashara kwa kiasi kikubwa kwani zaidi ya hapo, msafiri ataruhusiwa kubeba mzigo wa tatu wenye kilo 23 kwa daraja la uchumi na kilo 32 kwa daraja la biashara.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa gharama ya tiketi inajumuisha pia kodi inayolipwa katika  uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ambao hutumika na ndege za shirika hilo.


Zinazohusiana: 


Mfanyabiashara wa Kariakoo, Mathias Lufunzo ambaye amekuwa akitumia usafiri wa ndege za Emirates amesema ofa hiyo itampa ahueni kidogo kwa sababu amekuwa akitumia Dola za Marekani 800 (Sh1.840 milioni) kwa tiketi ya kwenda na kurudi. 

“Ninatumia takriban Dola 800 kwa tiketi ya kwenda na kurudi Dubai. Kama mfanyabiashara ninaangalia kama kuna haja ya mimi kwenda ili faida yote isijeishia kwenye safari,” amesema Lufunzo.

Kutokana na gharama hizo za usafiri, mara kadhaa amelazimika kununua bidhaa mtandaoni na kuzisafirisha hadi Tanzania. 

Hata hivyo, wafanyabiashara wameliomba shirika hilo kuwa na muendelezo wa ofa hizo kwani zitasaidia kusafiri kwenda katika nchi mbalimbali ikiwemo Japan na China kufuata bidhaa ili wazione kwa macho na kuachana dhana ya kununua kupitia mtandaoni. 

“ofa ni nzuri, waifanywe walau kila mwaka ili tusafiri tuchague vitu kwa macho na mikono. Saa zingine unaona kitu kwenye picha kinakuvutia lakini ubora wake sio mzuri,” Amesema Emanuel Munisi ambaye ni mfanyabiashara wa jijini Mwanza ambaye husafiri mara kwa mara kuelekea Dubai na China kwa ajili ya manunuzi hayo.