Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737 Max 8
Hatua hiyo imekuja baada ya tangu ndege yake aina ya Boeing 737 Max 8 kupata ajali jana (Machi 10, 2019) na kusababisha vifo vya watu 157.
- Hatua hiyo imekuja baada ya ndege yake aina ya Boeing 737-8 Max 8 kupata ajali jana (Machi 10, 2019) na kusababisha vifo vya watu 157.
- China nayo imeyaamuru mashirika ya ndege ya ndani ya nchi hiyo kusimamisha matumizi ya ndege aina ya Boeing 737 Max 8 kufuatia ajali hiyo.
Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari za ndege zake zote aina ya Boeing 737 Max 8 baada ya moja ya ndege zake kupata ajali jana (Machi 10, 2019).
Ndege hiyo iliyokuwa ikitokea jijini Addis Ababa kuelekea Nairobi, Kenya ilikuwa imebeba abiria 149 na wafanyakazi wanane na watu wote walio kuwa ndani ya ndege hiyo walifariki dunia, muda mfupi baada ya kuruka katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Addis Ababa Bole.
Katika taarifa iliyotolewa leo (Machi 11, 2019) na shirika hilo inaeleza kuwa wameamua kusitisha safari mpaka pale taarifa nyingine itakapotolewa baadaye, ikiwa ni tahadhari ya matumizi ya ndege hizo.
“Japo hatujui chanzo cha ajali hiyo, tumeamua kusitisha safari zote za ndege hizo kama tahadhari ya dharura ya usalama,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Accident Bulletin no. 5 Issued on March 11, 2019 at 07:08 AM Local Time pic.twitter.com/rwxa51Fgij
— Ethiopian Airlines (@flyethiopian) March 11, 2019
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea mjini Nairobi nchini Kenya ambapo ilianguka katika kiji cha Tulu Fara nje kidogo ya mji wa BIshoftu ikiwa ni kilomita 60 Kusini Magharibi mwa mji mkuu wa Ethiopia.
Soma zaidi:
- Airbus yatundika daruga kutengeneza ndege za kifahari za Airbus A380 Superjumbo
- Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’
- Hatua zitakazokusaidia umalize mchakato wa ‘Airport’ bila usumbufu
Tayari China imeyaamuru mashirika ya ndege ya ndani ya nchi hiyo kusimamisha matumizi ya ndege aina ya Boeing 737 Max 8 kufuatia ajali iliyotokea Ethiopia na nyingine nchini Indonesia.
Miongoni mwa watu waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na watalii, wafanyabiashara na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakielekea kwenye mkutano nchini Kenya.
Kufuatia ajali hiyo, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali ya ndege ya hiyo kwa sababu imeathiri jumuiya yote ya wana usafiri wa anga duniani.
“Salamu za rambirambi ziende kwa familia za abiria na wafanyakazi wa ndege waliopoteza maisha. Ajali hii ya kusikitisha imeathiri jumuiya yote ya wana usafiri wa anga duniani. Tunasubiri majibu ya kiuchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo,” imeeleza taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TCCA, Hamza Johari.