October 7, 2024

Shughuli za utalii zafunguliwa kwa masharti mazito ulimwenguni

Nchi nyingine zimeanza kulegeza masharti ikiwemo kufungua vivutio ambavyo vilikuwa vimefungwa hapo awali kujikinga na Corona.

  • Mbali na Tanzania, kwa nchi za Afrika zinazoweza kufikika kitalii ni Zambia pekee ambayo haijafunga mipaka yake.
  • Hata hivyo, ni lazima upimwe na ukae katika karantini kwa siku 14.
  • Nchi zingine ni Iran, Cambodia na baadhi ya sehemu za Marekani ikiwemo Mexico.

Dar es Salaam. Wakati wa Serikali ya Tanzania ikiruhusu shughuli za utalii kuendelea, baadhi ya nchi duniani ikiwemo Korea Kusini pia zimeanza kulegeza masharti yaliyowekwa dhidi ya ugonja wa Corona (Covid-19) na kuruhusu watalii kuanza kuingia katika nchi zao. 

Tanzania ambayo ni nchi ya kwanza Afrika Mashariki kufanya hivyo, ilifikia maamuzi ya kufungua anga lake kuruhusu ndege za kimataifa Mei 18 huku ndege za watalii zikitarajiwa kuanza kuingia mwishoni mwa mwezi huu.

Nchi nyingine zimeanza kulegeza masharti ikiwemo kufungua vivutio ambavyo vilikuwa vimefungwa hapo awali kujikinga na Corona. 

Kati ya nchi hizo ni Israel ambayo imefungua fukwe zake ambapo watalii wanaruhusiwa kutembelea maeneo ya fukwe za bahari ilimradi wanapeana nafasi ya mita moja kati ya mtu mmoja na mwigine.

Nchi hiyo imeruhusu sehemu zote za utalii zikiwemo baa, migahawa, hoteli na hifadhi za Taifa zifunguliwe. Hata hivyo, kumbi za starehe za usiku  hazijaruhusiwa kufunguliwa. 

Katika sehemu zilizoruhusiwa, watu wote wanatakiwa kuvaa barakoa muda wote isipokuwa wakati wanakula na kuzingatia usafi.

Huko Mexico nchini Marekani pia wameruhusu vivutio vya utalii vifunguliwe. Kwa Mexico vivutio maarufu ni pamoja na mbuga  ya Xcaret na Mji wa zamani wa Coba  huku tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 zinatakiwa kuzingatiwa unapotembelea sehemu hizo.


Zinazohusiana


Sehemu nyingine ni nchi ya Cambodia barani Asia ambayo kwa mujibu wa tovuti ya Wonderlast, mtu anayeingia katika nchi hiyo atatakiwa kuonyesha vyeti vya kumthibitisha kuwa hana ugonjwa wa Covid-19.

Pia, mtalii atatakiwa kuonyesha mpango wake wa bima ya afya ambao unatakiwa kutopungua walau Sh115 milioni ili kuruhusiwa kufurahia vivutio vilivyomo nchini humo.

Mbali na Cambodia, nchi nyingine ambazo mipaka yake haijafungwa ni Iran na Korea Kusini hivyo kuwa kati ya sehemu ambazo bado unaweza kufanya utalii japo zote zitakulazimu upimwe Covid-19 mara baada ya kuingia.

Kwa upande wa Afrika, nchi nyingine inayoruhusu shughuli za utalii ni Zambia ambayo Wonderlast imesema mtalii yeyote lazima apimwe Covid-19 na ndipo ataruhusiwa kuingia nchini humo.

Pia, ni lazima mgeni yeyote akae katika karantini kwa siku 14 kabla ya kuruhusiwa kwenda popote. 

Hata hivyo, “Visa” zote za utalii nchini Zambia zimefutwa labda watakaotalii ni raia wa nchi hiyo na siyo wageni.