Shule 10 bora kidato cha sita 2021
Kisimiri imeshika nafasi ya kwanza kitaifa kama ilivyokuwa mwaka 2020
- Kisimiri imeshika nafasi ya kwanza kitaifa kama ilivyokuwa mwaka 2020.
- Shule ya Zakia Meghji ya mkoani Geita imeshika nafasi ya nane kutoka nafasi ya 27 mwaka 2020.
- Shule nane kati ya 10 ni za Serikali kama ilivyokuwa mwaka 2020
Dar es Salaam. Ni mwaka mwingine wa furaha kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyopo mkoani Arusha baada ya kuongoza kitaifa katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Dk Charles Msonde leo Julai 10,2021 visiwani Zanzibar kuwa Kisimiri iliyokuwa na wanafunzi 72 waliofanya mtihani huo imeongoza kitaifa ikifuatiwa na Kemebos ya mkoani Kagera.
Shule hizo mbili zimeendelea kung’ang’ania katika nafasi hizo mbili kama ilivyokuwa mwaka 2020 huku kila moja ikipambana kumshusha mwenzake.
Kisimiri ni miongoni mwa shule nane za Serikali zilizoingia kwenye 10 bora mwaka huu ikiwa ni idadi sawa na shule kama hizo zilizoingia kwenye orodha hiyo ya dhahabu mwaka jana.
Upekee mwingine wa Kisimiri ni kuwa haijawahi kutoka kwenye kundi la shule 10 bora kitaifa tangu mwaka 2012 ambapo ilishika nafasi ya tatu kitaifa.
Nyingine zilizofanikiwa kuingia kwenye orodha hiyo kwa mujibu wa Dk Msonde, ni Dareda ya Manyara katika nafasi ya tatu kutoka nafasi ya 10 mwaka jana.
Tabora Girls katika nafasi ya nne ikipanda nafasi moja kutoka ya tano sambamba na kaka zao Tabora Boys iliyoshika nafasi ya tano ambazo zote ni shule kongwe nchini zilizopo katika mkoa wa Tabora.
Shule ya Feza Boys kutoka mkoani Dar es Salaam imeshika nafasi ya sita, ikifuatiwa na Mwandeti kutoka Arusha iliyoshika nafasi ya saba ikipanda nafasi mbili zaidi juu kutoka nafasi ya tisa mwaka jana.
Zakia Meghji kutoka mkoani Geita imeshika nafasi ya nane kitaifa kutoka nafasi ya 27 iliyoshika mwaka 2020, huku shule ya Kilosa ya Morogoro ikishika nafasi tisa kitaifa ikiwa imepanda nafasi tisa kutoka nafsi ya 18 mwaka jana.
Shule ya 10 kitaifa ni shule ya Mzumbe kutoka mkoani Morogoro ikiwa imeporomoka nafasi sita kutoka nafasi ya nne mwaka 2020.
Kati ya shule 10 vinara katika matokeo ya kidato cha sita 2021, mikoa ya Arusha, Morogoro na Tabora imeingiza shule mbili mbili huku mikoa ya Kagera ,Geita, Dar es Salaam na Manyara kila moja imeingiza shule moja.