Siku 21 kutoa hatma ya magazeti yaliyoshindwa kuhuisha usajili Tanzania
Imesema iwapo yatashindwa kuhuisha leseni zao ndani ya muda huo watapewa adhabu kali ikiwemo kufungiwa.
- Imesema iwapo yatashindwa kuhuisha leseni zao ndani ya muda huo watapewa adhabu kali ikiwemo kufungiwa.
- Kuna magazeti 18 ambayo hayajahuisha usajili wao tangu mwaka jana yakiwemo Raia Mwema, Uhuru na Mzalendo.
Dar es Salaam. Serikali imetoa siku 21 kwa magazeti ambayo yameshindwa kuhuisha leseni zake na kwamba iwapo yatashindwa kufanya hivyo ndani ya kipindi hicho yatayachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuyafungia.
Hatua hiyo ya Serikali imetangazwa na Idara ya Habari Maelezo kupitia ukurasa wake wa Twitter na kuthibitishwa na Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi.
“Idara ya Habari yawapa siku 21 kuanzia leo (Oktoba 10, 2019) wamiliki wa magazeti ambao hawajahuisha leseni zao. Hatua za kisheria kuchukuliwa ikiwemo kuyafuta na wamiliki kuanza kufikishwa Mahakamani,” imesema twiti hiyo iliyoambatanishwa na kiunganishi cha orodha ya magazeti hayo.
HABARI YA HIVI PUNDE: Idara ya Habari yawapa siku 21 kuanzia leo wamiliki wa magazeti ambao hawajahuisha leseni zao. Hatua za kisheria kuchukuliwa ikiwemo kuyafuta na wamiliki kuanza kufikishwa Mahakamani.
Orodha kamili imeambatishwa hapa:https://t.co/NeKXh34XTs
— Maelezo News (@maelezonews) October 10, 2019
Katika orodha hiyo, kuna magazeti 18 ambayo hayajahuisha usajili wao tangu mwaka jana yakiwemo Raia Mwema, Uhuru na Mzalendo. Magazeti mengine matano hayajahuisha usajili wao mwaka huu.
“Hii notisi inawahusu wale tu ambao muda wa kuhuisha usajili umeshapita na walishindwa kufanya hivyo mapema. Wale ambao muda wao (wa kuhuisha bado) hii notisi ni “reminder” (inakumbusha) ili wafanye hivyo mapema,” Dk Abbasi ameiambia www.nukta.co.tz.
Serikali imekuwa ikikosolewa vikali na baadhi ya wanaharakati kuwa inakandamiza uhuru wa habari nchini.
Hata hivyo, Serikali imepinga madai hayo na kueleza kuwa vyombo vya habari nchini vipo huru kutekeleza shughuli zao na kwamba hakuna chombo kilichominywa.