Siku ya Kutokomeza Umasikini Duniani ilivyogeuzwa kuwa Siku ya VICOBA Tanzania
Huadhimishwa Oktoba 17 kila mwaka kuhamasisha na kuendeleza mifumo ya vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi.
- Huadhimishwa Oktoba 17 kila mwaka kuhamasisha na kuendeleza mifumo ya vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi.
- Upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia vikundi vya kifedha vya kijamii umeongezeka kutoka asilimia 12 ya watanzania mwaka 2013 hadi asilimia 16 mwaka 2017.
Dar es Salaam. Oktoba 17 ya kila mwaka ni Siku ya Kutokomeza Umaskini Duniani. Mataifa mbalimbali ulimwenguni kote huadhimisha siku hiyo kwa kutathmini jitihada mbalimbali zilizofanywa katika kuboresha maisha ya wananchi hasa waishio vijijini.
Kutokana na mchango mkubwa wa vikundi vya kifedha vya kijamii (VICOBA) katika kutoa huduma za kifedha kwa wananchi na kuwezesha kuchangia katika kupambana na umaskini, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeona ni vema siku hiyo iwe pia Siku ya VICOBA Tanzania.
Lengo la kuwa na maadhimisho hayo ni kutambua, kuhamasisha na kuendeleza mifumo ya vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi na kutokomeza umaskini nchini.
Mchango wa VICOBA katika huduma jumuishi za kifedha nchini umeendelea kuongezeka kila mwaka ikiashiria kuwa watu wengi wanafikiwa na huduma za kifedha ili kuboresha maisha yao.
Ripoti ya utafiti wa hali ya huduma za kifedha Tanzania (FinScope) ya mwaka 2017 inaonesha kuwa upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia vikundi vya kifedha vya kijamii umeongezeka kutoka asilimia 12 ya watanzania mwaka 2013 hadi asilimia 16 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia nne kwa miaka minne.
Hali hiyo inamaanisha kuwa hadi mwaka 2017 watu zaidi ya milioni 4.4 walikuwa wanapata mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi kupitia vikundi vya kifedha vya kijamii ikilinganishwa na watu milioni 2.9 mwaka 2013.
Takwimu za maendeleo ya vikundi vya kifedha vya kijamii zilizopokelewa na NEEC hadi Aprili 2018 kutoka katika mikoa 21 (Halmashauri 147) kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara zinaonesha kuwa katika mikoa hiyo kuna vikundi vya kifedha vya kijamii 56,536 vyenye wanachama 859,656.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi mwaka 2018, vikundi hivyo vinasajiliwa katika Halmashauri za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambapo katika vikundi vilivyotolewa taarifa vikundi 41,020 vilikuwa vimesajiliwa na vikundi 13,589 vilikuwa bado havijasajiliwa.
Zinazohusiana:
- Idrisa Magesa: Kijana aliyerithi mikoba ya kuuza uji kutoka kwa bibi yake.
- Wavuvi watahadharishwa kupungua samaki Ziwa Victoria
- Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
Kutokana na umuhimu wa vikundi hivyo kwa jamii, vimeendelea kujiimarisha kiuchumi na kuongeza mitaji na mikopo inayowafikia wanachama ambao huwekeza katika biashara na viwanda vidogo vidogo ili kujikwamua kimaisha.
“Hadi kufikia Aprili 2018 vikundi hivyo kwa ujumla vilikuwa na mtaji wa shilingi 84.91 bilioni na viliweza kutoa mikopo ya shilingi 44.46 bilioni kwa wanavikundi,” inaeleza taarifa ya NEEC.
Licha ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Kifedha ya Mwaka 2017 kuvitambua vikundi vya kifedha vya kijamii kama moja ya nyenzo muhimu ya kufikisha huduma za kifedha kwenye jamii, hususan maeneo ya vijijini, bado zipo changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji ufumbuzi wa kudumu.
Mathalani, kutoa huduma za kimtaji kwa makundi maalum kwa wanaoanza biashara na biashara zinazogusa wanufaika wengi kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, inashauriwa kuimarisha sekta ya fedha ili kuhudumia sekta binafsi kwa kuongeza utoaji wa huduma mbalimbali za kifedha kwa gharama nafuu ili kuwafikia watu wengi na kuondokana na umasikini wa kipato.
“Kujenga utashi wa kijasiriamali huku tukizikabili changamoto za kitamaduni hasa zilezinazokandamiza wanawake wajasiriamali,” inaeleza taarifa ya NEEC.
Kutoa fursa kwa wadau wa vikundi vya kifedha vya kijamii kukutana, kubadilisa uzoefu na kuhamasishana kujiunga katika vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana na kuwawezesha vijana na wanawake kuelewa umuhimu wa mapambano dhidi ya umaskini kwa kujenga tabia ya kujiwekea akiba kupitia vikundi.
Kupunguza changamoto za kiutawala wa uanzishaji na uendelezaji wa biashara na ujasiriamali hasa katika urasimishaji, upatikanaji wa taarifa, gharama za za urasimishaji na mikataba.