Simiyu watakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji wa pamba
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao la pamba sambamba na mazao mengine ya biashara ili kuwa na uhakika wa mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka (aliyesimama) akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ( aliyekaa kulia) wakati wa kikao cha wadau wa zao la pamba mjini Simiyu leo. Picha|Wizara ya Kilimo.
- Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema itawasaidia kuwa na uhakika wa mapato.
- Watakiwa pia kuangazia kilimo cha mkonge na korosho.
- Wakulima wa pamba waitaka Serikali iwalipe fedha zao.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao la pamba sambamba na mazao mengine ya biashara ili kuwa na uhakika wa mapato.
Katibu Mkuu huyo amewasihi viongozi wa mkoa huo kuwahamisha wakulima pamoja na kuzalisha zao la pamba watumie ardhi iliyopo kuzalisha zao la mkonge na korosho yanayoweza kustawi vizuri kwenye mkoa huu.
“ Nawashawishi wakulima wa Simiyu pamoja na kulima pamba kwa wingi pia walime mkonge pia kwani tunacho kituo chetu cha TARI Mlingano (kilichopo Muheza mkoani Tanga) chenye uwezo wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora za mkonge hadi hapa,” amesema Kusaya leo mjini Bariadi na wakati aliopongea na wanunuzi wa zao la pamba katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Simiyu Anthony Mtaka.
Kusaya amesema anatambua uwepo wachangamoto za madai ya baadhi ya wakulima wa zao la pamba pamoja na halmashauri kutokana na ushuru kutolipwa na kuwa Serikali inatafuta suluhu ya jambo hilo.
Amewataka wanunuzi wa zao la pamba kuendelea na maandalizi ya msimu ujao unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Mei na kuwa Serikali inaendelea kushughulikia madai hayo.
Soma zaidi: Wakulima kuuza pamba kwa bei wanayoitaka
Katika kikao hicho Kusaya aliwaomba viongozi wa mkoa wa Simiyu kushirikiana wizara ya Kilimo kutengeneza mazingira mazuri ya wakulima kuendelea kunufaika na kazi zao kwa kupata soko la uhakika.
Mtaka amesema mkoa wake ndio unaoongoza nchini kwa uzalishaji wa pamba na kuwa wakulima wana imani na Serikali katika kuhakikisha wanapata fedha zao zilizosalia
Amesema Sh3.5 bilioni bado hazijalipwa kwa halmashauri za mkoa wake kama ushuru wa mazao kutoka kwa wanunuzi na Sh794 milioni inadaiwa na wakulima hadi sasa.
Mkoa wa Simiyu katika msimu wa mwaka 2018/2019 ulizalisha kilo milioni 166.19 za pamba na kuufanya ushike nafasi ya kwanza kitaifa.