July 5, 2024

Simu zachangia kushuka kwa redio majumbani Tanzania

Hadi kufikia mwaka 2017/18 zaidi ya nusu ya kaya za Tanzania zilikuwa hazimiliki redio.

  • Hadi kufikia mwaka 2017/18 zaidi ya nusu ya kaya za Tanzania zilikuwa hazimiliki redio.
  • Mabadiliko ya teknolojia ikiwemo simu za mkononi zimechangia kupunguza umiliki wa redio.
  • Lakini bado Watanzania wanaamini redio kama chanzo muhimu cha kupata taarifa.  

Dar es Salaam. “Zamani ilikuwa fahari kumiliki redio kwa sababu ndiyo tulikuwa tunapata taarifa zaidi siyo kama sasa hivi,” anasema Mzee Oberd Mwalubuli, mkazi wa jijini Mbeya ambaye ni miongoni mwa watu ambao kwa sasa hawezi tena kujisikia fahari kumiliki redio. 

Mzee huyo mwenye miaka 79 anasema enzi zao hasa miaka ya 1970 watu wachache walikuwa wana uwezo wa kumiliki redio na ilikuwa moja ya kifaa adimu cha mawasiliano ikizingatiwa kuwa kulikuwa hakuna simu za mkononi. 

“Mimi nilikuwa nafanya kazi kwenye kiwanda cha sabuni cha Hisoap, kwa hiyo niliweza kununua redio kubwa ya “National” ambayo ilinisaidia kupata habari na majirani zangu walikuja kusikiliza kwangu hasa ikifika saa 2 usiku,” amesema Mwalubuli. 

Hata hivyo, mzee huyo hakujua kama ipo siku ambayo redio haitakuwa kifaa cha thamani katika kaya nchini Tanzania kwa sababu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yameongeza wigo wa watu kupashana habari.

Licha ya mabadiliko hayo, redio imekuwa kifaa muhimu kinachowezesha watu kupata habari, elimu na burudani zinazowasaidia kufanya maamuzi juu ya maisha yao ya kila siku. 

Wakati idadi ya vituo vya redio ikiongezeka nchini Tanzania, kaya zinazomiliki redio inazidi kupungua kila mwaka.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo ya kwanza ya mwaka 2020 zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2019 Tanzania ilikuwa na vituo vya redio 183 vikiwa vimeongezeka kutoka 158 mwaka 2018. 

TCRA katika takwimu hizo inaeleza kuwa vituo vya redio nchini vimekuwa vikiongezeka kila mwaka kwa viwango tofauti tangu mwaka 2014.

Hata hivyo, ongezeko hilo halishabiani na kaya ambazo zinamiliki redio ili kupata matangazo ya vituo hivyo vya redio vya umma na binafsi ambazo zimesambaa katika maeneo mbalimbali Tanzania. 

Ripoti ya Takwimu muhimu za Tanzania (Tanzania in Figure 2019) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Juni mwaka huu inaeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2017/18 asilimia 43 ya kaya za Tanzania Bara ndiyo zilikuwa zinamiliki redio kutoka asilimia 55 mwaka 2011/12. 

Hii ina maana kuwa umiliki wa redio umepungua kutoka kaya 55 kati ya 100 mwaka 2011/12 hadi kaya 43 mwaka 2017/18. 

Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya nusu ya kaya za Tanzania Bara hazimiliki redio kabisa. Wakati idadi ya kaya zinazomiliki radio zikipungua, kaya zinazomiliki simu za mkononi imekuwa ikongezeka ambapo ripoti hiyo inaeleza kuwa hadi mwaka 2017/18 zaidi ya robo tatu au asilimia 78 ya kaya Tanzania Bara zilikuwa zinamiliki simu za mkononi. 

Kwa lugha rahisi ni kwamba kwa sasa kaya tatu kwa kila nne zilizopo Tanzania Bara zinamiliki simu ya mkononi.

Uwepo wa redio ndani ya simu hasa masafa ya FM, umewafanya watu wengi kuachana na redio za nyumbani au za kushika mkononi. 

Wadau wa habari na teknolojia wanaeleza kuwa kwa sasa watu wengi wanasikiliza matangazo ya redio kwa njia ya simu za mkononi na kupata habari kwa njia ya mitandao ya kijamii. 

Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena ameiambia Nukta kuwa mabadiliko ya teknolojia ikiwemo mitandao ya kijamii yamerahisisha upatikanaji wa taarifa, jambo linalowafanya watu wasitegemee tu redio za nyumbani kupata habari. 

“Malengo ya kuanzisha redio hutofuatiana, jambo linaloweza kuwafanya wasikilizaji kutafuta namna nyingine ya kupata habari kwa haraka na urahisi,” amesema Meena. 


Zinazohusiana:


Hata wakati umiliki wa redio ukipungua katika ngazi ya kaya, bado wananchi wengi wanaamini redio kama chanzo muhimu cha kupata taarifa. 

Ripoti ya utafiti wa mtazamo wa wananchi kuhusu demokrasia utawala bora na uchumi wa mwaka 2017 uliotolewa na taasisi ya Afrobarometer na taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (REPOA) inaeleza kuwa takriban nusu au asilimia 45 ya Watanzania wanaamini kuwa redio ndiyo chanzo muhimu cha kupata taarifa. 

Mtaalamu wa programu za kompyuta, Emmanuel Feruz amesema kupungua kwa kaya zinazomiliki redio haimaanishi kuwa watu hawasikilizi redio lakini kinachotokea wanatumia mifumo mingine ya teknolojia.

“Watu wengi wanasikiliza redio za mtandaoni kwa sababu wana intaneti na simu janja, hawawezi tena kusubiria redio za nyumbani kupata taarifa,” amesema Feruz.

Picha ya mbele|BBC Africa