November 24, 2024

Simulizi ya walimu wanavyokabiliana na uhaba wa makazi Mbeya

Wanatamani Serikali na wamiliki wa daladala wangeanzisha utaratibu wa kutolipisha nauli kwa walimu kama ilivyo Dar.

  • Wanatamani wangekuwa hawalipi nauli kama walimu wa Dar es Salaam.
  • Kuna baadhi ya walimu wanasafiri umbali wa takriban kilomita 26 kufika shuleni.
  • Wadau washauri sekta binafsi ijitose kuokoa jahazi.

Mbeya. Licha ya kufanyaka kazi katika moja ya shule kongwe mkoani Mbeya, walimu wa Shule ya Msingi Iyela iliyopo  kata ya Iyela jijini Mbeya hawajawahi kubahatika kuishi kwenye makazi rasmi yaliyojengwa kwa ajili yao.

Sehemu kubwa ya walimu wa shule hiyo yenye miaka 67 kwa sasa wanaishi mbali na kituo chao cha kazi jambo linalowaongezea gharama za maisha kwa kuwa wanalazimika kutumia usafiri zaidi ya mmoja.

Kwa mwalimu anayeishi mjini hadi kufika shuleni hapo atalazimika kupanda bajaji au bodaboda na iwapo katika safari hiyo atakuwa pekee yake anaweza hata kutumia wastani wa Sh 4000 kwa siku, kiwango ambacho ni  kikubwa kuliko nauli ya kutoka Mbeya Mjini hadi Tukuyu ambayo ni Sh3,000. Tukuyu ipo umbali wa kilomita 70 kutoka Mbeya Mjini. 

“Huku ni changamoto hakuna magari yanayofika hapa hivyo ukishuka kwenye gari lazima uchukue bajaj au bodaboda. Pia, hakuna hata mgahawa unaouza chakula karibu na shule,” anasema Salome Mwakilingili, Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Iyela.

Kutokana na kuwepo kwa gharama kubwa za usafiri, baadhi ya walimu wanashauri Serikali na wamiliki wa daladala mkoani humo wafanye utaratibu kama wa Dar es Salaam ambao unawapa fursa walimu kutolipa nauli wanapoenda kazini.

“Huku bora hata wangeanzisha utaratibu kama wa Dar es Salaam tupande bure daladala kwa kuwa tunatoka mbali hadi kuja kufundisha huku shuleni,” anasema Mary Haule, Mwalimu wa Chekechea wa shule hiyo.

Je, ni kweli shule hiyo haijawahi kuwa na nyumba za walimu tangu ukoloni?

Hapana shaka kuwa shule hiyo iliwahi kuwa na nyumba za walimu. Hadi sasa kuna ushahidi wa nyumba moja ya walimu iliyogeuka gofu. 

Hata hivyo, Nukta hakuna taarifa za kina juu ya nini kilitokea. Walimu wengi waliopo kwa sasa ni wageni hawajui historia kuhusu nyumba hizo na hawafahamu sababu ya shule hiyo kukosa makazi  licha ya kuanzishwa mwaka 1951. 

“Hakuna nyumba hata moja ya mwalimu kwa sasa. Iliyopo ni nyumba ya zamani ambayo hakuna mtu anayeweza kuishi mahali hapo hivyo walimu wote wanaishi mbali na shule,” anasema Mwajabu Mzava, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo.

Pamoja na changamoto hizo, walimu wa shule hiyo wanaonekana kujituma kufundisha baada ya kufanya vizuri katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi (PSLSE) mwaka 2017 kwa kuwa ya nane kati ya shule 76  za jiji la Mbeya na ya 15 kimkoa kati ya shule 495.


Jiandae kwa masomo ya elimu ya juu kwa kufahamu sifa za kujiunga na kozi unayoipenda. Tembelea Elimu Yangu


Changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu ni kubwa na inazikabili shule nyingi za mkoa huo ukiachana na Iyela. Hali iliyopo katika shule hiyo haitofautiana sana na ile iliyopo katika shule za Iyunga, Ikuti, Jitegemee na Nzovwe ambazo Nukta ilibahatika kuzitembelea katikati ya Mei 2018.

Shule ya Msingi Iyunga iliyoanzishwa mwaka 1975 nayo ina nyumba moja tuu ya walimu huku walimu wote 21 wakiwa wakikaa nje ya shule.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Iyunga, Adela Athuman anasema ukosefu wa nyumba za walimu ni changamoto kwao ikizingatiwa “mshahara huo huo mdogo unatakiwa ukatwe kodi, nauli bado hujala na unajikuta umepanga mtaani mbali na shule.”  

“Naishi Mbalizi na sio mjini huko Utengule. Mimi nakaa mbali kuliko walimu wote hapa. Natembea kama kilomita tatu ili nifike stendi nipande daladala. Nikishuka Iyunga natembea au napanda bodaboda hadi shuleni,” anasema Siwagwe Msasi, Mwalimu darasa la tatu shule ya msingi Inyala ambaye amefundisha shuleni hapo tangu mwaka 2009.

Msasi anasema hali hiyo inawakumba licha kuwepo malimbikizo ya fedha za likizo, ukosefu wa motisha au mafunzo mbalimbali kwa walimu ili waweze kuendana na kasi ya kubadilisha mitaala ya kufundishia mashuleni.

“Unakuta shule nzima wanapelekwa walimu wawili au watatu mafunzoni na wengi tunakuwa bado hatujajifunza mbinu mpya za ufundishaji, hivyo nashauri serikali iangalie upya mafunzo kwa walimu yawe yanatolewa siku ya likizo au wakufunzi wawe wanakuja kuyatolea mashuleni,” anasema Msasi.

                                      Shule ya msingi Inyala inavyoonekana kwa mbele. Picha| Zahara Tunda

Uchambuzi wa takwimu za msingi za elimu Tanzania (BEST) mwaka 2016 unabainisha kuwa Halmashauri ya jiji la Mbeya linakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu 1,762 huku zilizopo ni nyumba 103 tuu.

“Mimi ningeshauri Serikali ijenge nyumba za walimu mashuleni hii itawasaidia sana walimu kuokoa gharama na kuwahi kufundisha kwa kuwa wengine wanakaa mbali sana na wanalazimika kupanda bodaboda,” anasema Allen Gibson, Dereva wa bodaboda katika kituo cha Iyunga jijini hapa ambaye husafirisha walimu mara kwa mara.

Baadhi ya wadau wanaushauri kuwa pamoja na kuwa Serikali ndiyo yenye jukumu kubwa la kujenga makazi ya watumishi wa umma kuna ulazima wa sekta binafsi kujitosa kusaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu.

“Ni wakati wa Serikali kushirikisha sekta binafsi katika kuendeleza elimu kwa kusaidia ujenzi wa nyumba za walimu. Nguvu iliyoelekezwa katika kutoa elimu bure ingehamishiwa pia katika ujenzi wa nyumba za walimu na kuboresha maslahi yao,” anasema Gilbert Gozibert, Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Jamii isikwepe majukumu”

Kwa upande wa serikali juhudi za kuendeleza shule na nyumba za walimu bado zinaendelea kusuasua kutokana na rasilimali fedha zilizopo kuhitajika kutatua changamoto nyingi zilizopo katika sekta ya elimu mkoani humo.

Afisa Elimu mkoa wa Mbeya, Pauline Ndigeza anasema; “wadau wote wa elimu na wazazi tukae pamoja tuweze kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazoizunguka sekta ya elimu kwa sababu Mbeya wanafunzi ni wengi ila miundombinu ni michache.”